Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Wakfu ya Yemen, katika mji mkuu Sana’a maeneo ya kihistoria na misikiti iliyoharibiwa katika hujuma ya ndege za kivita za Saudia ni zaidi ya 283.
Wizara ya Wakfu ya Yemen imetoa ripoti inayoonyesha idadi ya misikiti na majengo ya turathi ya kihistoria yaliyoharibiwa katika hujuma ya muungano vamizi wa Saudia ni zaidi ya 1,050 kote Yemen.
Taarifa hiyo imesema baadhi ya majengo yaliyoharibiwa yaliyejngwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita. Ripoti hiyo aidha imesema wafanyakazi 100 wa Wizara ya Wakfu wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo ya Saudia dhidi ya taifa la Yemen.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.
Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 17,000 wanaripotiwa kupoteza maisha moja kwa moja katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen huku makumi ya maelfu yaw engine wakipoteza maisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.