IQNA

Onyo Kali la Majeshi ya Iran kwa wanaovuruga usalama wa eneo

22:32 - April 28, 2020
Habari ID: 3472712
TEHRAN (IQNA)- Vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiisamu ya Iran vilitoa taarifa na kuonya kwamba: Kuundwa miungano ya urongo kwa uongozi wa Marekani kwa kizingizio eti cha kusimamia usalama wa meli ni hatua ya hatari na wakati huo huo inavuruga amani na usalama wa eneo.

Taarifa hiyo ya Jumatatu imeeleza wazi kwamba: "Harakati za Marekani zenye hatari na hatua yake ya kuanzisha vituo vya kijeshi katika eneo hili la Asia Magharibi kivitendo ndio chimbuko la ukiukaji wa sheria, ushari na ukosefu wa amani; na Iran imebainisha katika majukwaa ya kimataifa muamala huu wa Marekani ambao unavuruga amani na usalama na ambao kimsingi unakinzana kikamilifu na sheria na kanuni za kimataifa."

Taarifa ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiisamu ya Iran  imesisitiza kuwa, mbadala pekee na wa uhakika wenye kuweza kudhamini amani na uthabiti katika Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormuz na Bahari ya Oman ni kuondoka vikosi vya Marekani na washirika wake ambao kimsingi ndio kitovu cha uvurugaji amani na usalama na kisha kukabidhi usimamiaji wa usalama kwa nchi za eneo hili ambazo zitafanikiwa kusimamia usalama huo kupitia ushirikiano baina yao.

Weledi wa mambo wanasema taarifa ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiisamu ya Iran imebeba ujumbe wa wazi kabisa katika uwanja huu na unabaisha bayana kwamba, chokochoko ya aina yoyote ile, hatua za maudhi na za kichochezi zitakabiliwa na majibu makali ya vikosi vya ulinzi vya taifa hili ambapo madhara yake yatavikumba vikosi vya adui vikiwemo vya Marekani.

3894794

captcha