IQNA

Indhari ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuenea COVID-19 nchini Yemen

11:24 - April 30, 2020
Habari ID: 3472718
TEHRAN (IQNA) –Nchini Yemen kumeripotiwa kesi kadhaa za ugonjwa wa COVID-19 au corona Jumatano huku Umoja wa Mataifa ukibainisha wasiwasi wake kuwa ugonjwa huo yamkini unaenea katika nchi hiyo bila kujulikana huku mamilioni wakikabiliwa na njaa na ukosefu wa huduma za afya.

Kesi tano mpya za COVID-19 zimeripotiwa katika mji wa bandarani wa Aden ambao ni makao ya wapiganaji wanaofungamana na rais aliyepinduliwa nchini humo Abdu Rabbuh Mansour Hadi.

Siku ya Jumatano Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa ugonjwa wa COVID-19 unaenea katika jamii. Wafanyakazi wa sekta ya afya wanasema ugonjwa wa COVID-19 unaweza kuenea haraka katika nchi hiyo yenye watu milioni 24 ambao miongoni mwao, asilimia 80 wanategemea msaada wa chakula na milioni 10 wanakabiliwa na hatari ya baa la njaa.

Hayo yanajiri wakati ambao Baraza la Mpito la kusini mwa Yemen ambalo linapata uunga mkono wa Umoja wa Falme za Kiarabu Jumapili lilitangaza kuwa mikoa ya kusini mwa Yemen itakuwa na serikali zenye mamlaka ya kujitawala.

Tayari misikiti imeshafungwa kote Aden ili kuzuia ugonjwa wa COVID-19 kama ambavyo pia kuna amri ya kufunga maduka na migahawa kwa muda wa wiki mbili. Aidha masoko yanayouza miraa yamefungwa kwa muda usiojulikana baada ya majimbo yote ya kusini kupiga marufuku uuzaji wake mijini.

Katika kukabiliana na corona Yemen inakumbana na matatizo makubwa kama vile uhaba wa mashine za kupumua, vitanda vya vitengo vya ICU na mitungi ya oxigeni. Sambamba na hali hiyo ya kusikitisha Saudi Arabia imekiuka madai yake ya usitishwaji vita Yemen na inaendelea kudondosha mabomu katika nchi hiyo masikini zaidi Asia Magharibi.

3895413

captcha