Kuanzia Oktoba Mosi mwaka jana, Iraq ilianza kushuhudia maandamano ya wananchi, ambapo baadaye yalibadilika na kuchukua sura ya utumiaji mabavu baada ya makundi ya ndani na ya nje yenye chuki na taifa hilo kuingilia kati na kutaka kunufaika na anga iliyokuwa imejitokeza. Hatimaye matukio hayo yalipelekea kujiuzulu Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi Novemba 29 mwaka jana. Katika kipindi hiki, Rais Barham Salih wa Iraq aliwatambulisha shakhsia watatu kwa nyakati tofauti na kuwapa jukumu la kuunda Baraza la Mawaziri. Wanasiasa wawili wa awali ambao ni Muhammad Tawfiq Allawi na Adnan Zurfi hata hawakufikia hatua ya kwenda Bungeni na kuwasilisha orodha yao ya mawaziri kwani walijitoa katika hatua za awali.
Mustafa al-Kadhimi, Mkuu wa Shirika la Intelijensia la Iraq ni shakhsia wa tatu aliyeteuliwa na Rais Barham Salih kwa ajili ya kuunda serikali mpya. Kutokana na makundi karibu yote ya kisiasa ya Iraq kuonyesha kumuunga mkono al-Kadhimi ilitabiriwa kuwa, baraza lake la mawaziri lingepata kura ya Bunge ya kuwa na imani nalo.
Baada ya serikali yake kuridhiwa na Bunge la Iraq, kivitendo kipindi cha muda cha serikali ya mshikizo ya Adil Abdul-Mahdi nacho kimefikia tamati na mkwamo wa kisiasa wa nchi hiyo uliodumu kwa miezi mitano nao takribani umemalizika.
Mawaziri 15 waliopata kura za kuwa na imani nao wanajumuisha mawaziri 9 Mashia, mawaziri 5 Masuni na waziri mmoja Mkurdi. Aidha mawaziri watano ambao hawajapata kura za kuwa na imani nao ni mawaziri wawili Mashia, mmoja Msuni, Mkurdi mmoja na waziri mmoja Mkristo. Kimsingi ni kuwa, waziri pekee wa dini za waliowachache nchini Iraq ameshindwa kupata kura ya kuwa na imani naye katika Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi. Suala muhimu ni kuwa, tofauti la ilivyokuwa katika Baraza la Mawaziri la Adil Abdul-Mahdi ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani hakupata kura ya kuwa na imani naye, katika baraza hili jipya waziri aliyependekezwa kushika wadhifa huo ameweza kupata kura za Wabunge za kuwa na imani naye.