Ayatullah Isa Qassim alisema hayo jana Jumatano kwa mnasaba wa siku ya kukumbuka kifo cha Imam Khomeini (MA), Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kubainisha kuwa, "Mapinduzi ya Imam Khomeini yalikuwa yanafanana na ya Mitume na yalifuata malengo yaliyoanzishwa na Mitume."
Mwanazuoni huyo maarufu wa Kiislamu nchini Bahrain amesema pamoja na kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yamekumbwa na njama nyingi za maadui, lakini yamefanikiwa kudumu na kuondokana na changamoto zote.
Ayatullah Isa Qassim ameashiria kuhusu siri ya kubakia hai na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kueleza bayana kuwa, "iwapo Mapinduzi si kwa ajili ya Allah na njia yake, katu hayatokuwa makubwa na kudumu. Mapinduzi ya Imam Khomeini hayakufungwa na wakati kutokana na malengo yake."
Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Milaadia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Hatimaye Mapinduzi hayo yalipata ushindi mwaka 1979.
Siku kama ya jana miaka 31 iliyopita, sawa na tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, mwafaka na tarehe 4 Juni 1989 Milaadia, Imam Ruhullah Khomeini (MA), Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia baada ya kuishi kwa miaka 87.