IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Maadui hawajaweza kufikia malengo yao dhidi ya Iran hata baada ya kuweka vikwazo vikali

17:16 - July 12, 2020
Habari ID: 3472957
TEHRAN (IQNA) -Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema adui amepoteza matumaini kutokana na namna taifa la Iran linavyokabiliana na kila harakati dhidi ya mfumo wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, kama ambavyo leo adui amekiri, pamoja na kuwepo vikwazo vikali zaidi na mashinikizo ya pande zote, hajaweza kufikia malengo yake dhidi ya Iran.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo katika mkutano alioufanya kwa njia ya video na wajumbe wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria ‘Msingi Imara na Uwezo wa Kimaada wa Nchi’ na ‘Uwezo wa Kimaanawi na Kiimani wa Taifa’ na kusema: “Tuna uhakika kuwa matatizo yote yaliyopo yanaweza kutatuliwa na Majilisi inapaswa kuiainisha vipaumbele sambamba na kujiepusha na masuala ya kando kando na wakati huo huo kufanya kazi kwa ikhlasi kwa ajili ya wananchi ili taathiria ihisike katika mchakato wa kutatua matatizo ya wananchi.”

Ayatullah Khamenei amesema bunge hilo la awamu ya 11 ndio bunge lenye nguvu zaidi na la kimapinduzi zaidi baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: “Uwepo wa vijana wenye motisha, waliojaa imani, wenye uwezo mkubwa, wenye elimu na watenda kazi pembizoni mwa wasimamizi wa kimapinduzi wenye uzoefu mrefu wa utendaji na pia uwepo wa wanasiasa waliowahi kuwa wabunge ni nukta ambazo zimelifanya Bunge la 11 kuwa bunge bora sana na lenye kuibua matumaini.”

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa, matatizo makubwa ya kiuchumi nchini ni kama ‘ugonjwa’ na kuongeza kuwa: “Kutokana na msingi imara na uwezo wa kujihami, bila shaka nchi hii itaweza kupata ushindi mkabala wa ‘ugonjwa’ huu.

Ayatullah Khamenei ameashiria baadhi ya uwezo wa nchi na kusema: “Kuasisiwa maelfu ya mashirika ambayo msingi wake ni elimu, kutekelezwa mamia ya miradi ya miundo msingi, kuzinduliwa bila kikomo miradi mipya ya maenedeleo, ustawi usio na kifani wa sekta ya kijeshi na mafanikio yenye kustahiki pongezi katika uga wa anga za mbali, yote hayo ni matokeo ya kutumia uwezo wenye nguvu wa ndani ya nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria ‘kushiriki mapema na kwa kujitolea wananchi katika kukabiliana na wimbi la kwanza la corona’ , ‘huduma yenye thamani kubwa ya taifa katika harakati ya msaada wa waumini kwa familia daifu katika jamii’ na ‘kushiriki kwa wingi wananchi katika kumuaga jenerali Soleimani’ na kusema, hiyo ni mifano ya uwezo wa kina wa kimaanawi wa taifa la Iran. Ayatullah Khamenei amesema kuwa: “Katika kuenzi ‘dhihirisho la nguvu ya kitaifa na jihadi’ la Wairani, yaani Shahidi Soleimani, wananchi wameonyesha kuwa wana imani katika mapambano na muqawama mkabala wa madola ya kiistikbari na kibeberu.

3909964

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha