IQNA

20:53 - June 24, 2020
News ID: 3472895
TEHRAN (IQNA)- Israel inashinikizwa na jamii ya kimataifa isitishe mpango wake wa kupora maeneo zaidi ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud na Benny Gantz kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe, walifikia makubaliano ya kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ifikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2020. Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuwadia muda wa kutekelezwa mpango huo, mashinikizo dhidi ya baraza la mawaziri la Israel yanaonekana kushadidi kila upande.

Ndani ya Israel kwenyewe (Palestina inayokaliwa kwa mabavu) kumeibuka mitazamo tofauti baina ya mawaziri. Netanyahu ambaye anasisitiza kutekelezwa mpango huo tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Julai, amemtishia Benny Gantz kwamba, atalivunja baraza la mawaziri na kuitisha uchaguzi wa nne wa bunge katika kipindi cha mwaka mmoja, endapo ataendelea kupinga utekelezwaji wa mpango huo.

Huko Palestina nako sambamba na kuweko mtazamo na msimamo mmoja baina ya makundi mbalimbali katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wa kupinga mpango huo, Nabil Abu Rudainah, msemaji rasmi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kuwa, taifa la Palestina limepambana kwa miaka mingi na katu halitaruhusu njama hii mpya itekelezwe. Wakati huo huo, wananchi wa Palestina wameendelea kuandamana wakilaani mpango huo wa Israel wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina.

Mashinikizo dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika uga wa kimataifa nayo yameshadidi mno. Katika upande mwingine malalamiko na matamshi ya ukosoaji dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mpango wa kutwaa ardhi ya Palestina yamegeuka na kuwa ya kivitendo ambapo wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Russia, China na wengine wa nchi kadhaa za Ulaya na Magharibi, juzi walishiriki katika maandamano ya maelfu ya waandamanaji jirani na lango kusini la kuingia katika mji wa Jericho.

Wakati huo huo, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Jumanne ya kuamkia jana lilipasisha “Azimio la Vitongoji” lililo dhidi ya Israel katika kikao chake 43.

Azimio hilo linataka kususiwa kazi mbalimbali za Israel zinazofanyika katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kama ambavyo linatahadharisha pia kwamba, watu watakaoshiriki katika shughuli hizo watapigwa faini kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Katika azimio lake jingine, Baraza la Haki za Binadamu limesisitiza haki ya Wapalestina ya kujiainishia mustakabali wao.

Katika hali ambayo, mashinikizo dhidi ya utawala haramu wa Israel kuhusiana na mpango wake wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubi wa za Palestina yameshadidi mno na hata kuna taarifa zilizoenea zinaoeleza juu ya kuakhirishwa mpango huo, serikali ya Marekani imeendelea kunyamazia kimya kadhia hiyo.

Mpango wa utawala haramu wa Israel wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ni miongoni mwa vipengee muhimu vya mpango wa kibaguzi wa “Muamala wa Karne”, kwani kwa mujibu wa mpango huo wa Kimarekani, ardhi zote zinazozozaniwa na Israel na mataifa ya Kiarabu zikiwemo za Palestina na Syria zimepatiwa utawala huo ghasibu.

Bado haijafahamika kama Benjamin Netanyahu atatoa jibu gani kwa upinzani wa kimataifa dhidi ya mpango wake wa kutwaa eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina. 

Hata hivyo haionekani kama kutekelezwa mpango huo kutakuwa ni mafanikio kwa Waziri Mkuu wa Israel, kwani kwanza, mizozo na mivutano ya ndani katika serikali yake inaongezeka siku baada ya siku; na pili makundi ya Palestina yana azma ya dhati na irada ya pamoja kwa ajili ya kuufanya mpango huo ugonge mwamba na kushindwa kufikia malengo yake.

3471778

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: