IQNA

Maulamaa Yemen wataka Waislamu duniani watetee Msikiti wa al-Aqsa na Haram Mbili tukufu

19:21 - July 17, 2020
Habari ID: 3472971
TEHRAN (IQNA) - Baraza la Maulamaa wa Yemen limeyatolea mwito mataifa ya Kiislamu wa kuyataka yatekeleze jukumu lao la kuuhami msikiti wa al-Aqsa na Haram Mbili tukufu za Makka na Madina katika kukabiliana na chokochoko za Wazayuni na utawala wa Aal Saud.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Masirah, baraza la maulamaa wa Yemen limeeleza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni uhaini mkubwa na fedheha ya kihistoria na kusisitiza kwamba, kutetea kadhia ya Palestina na harakati za Jihadi na muqawama ni wajibu wa kisharia na masuulia ya kidini kwa Waislamu wote duniani.

Baraza hilo la maulamaa wa Yemen vile vile limelaani jinai zilizofanywa na muungano vamizi wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia ya kushambulia maeneo ya raia katika mikoa ya Hajjah na al Jawf, ambayo imesababisha kuuawa shahidi makumi ya wanawake na watoto na limewataka wananchi wa Yemen na makabila ya nchi hiyo yasimame pamoja na kuchukua hatua ya kuwaadhibu wavamizi na kuwatimua katika ardhi ya nchi hiyo.

Siku ya Jumatano, ndege za kivita za muungano vamizi unaoongozwa na Saudia zilishambulia mkusanyiko wa sherehe ya harusi ya watu wa kabila la Bani Nawf katika eneo la al-Musaafah al-Maraaziq mkoani Jawf na kupelekea watu 25 kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, ambapo wengi wa waliouawa na kujeruhiwa ni wanawake na watoto wadogo.

3910955

captcha