IQNA

Mahakama Jordan yaamuru kuvunjwa Harakati ya Ikhwanul Muslimin

19:37 - July 17, 2020
Habari ID: 3472972
Mahakama ya Kilele ya Jordan imetoa hukumu ikitangaza kuvunjwa Harakati ya Ikhwanul Muslimin nchini humo.

Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Jordan ilianzishwa mwaka 1945 na ilitangaza waziwazi shughuli zake za kisiasa mwaka 1952 baada ya kubuniwa Katiba ya Jordan. Kundi hilo linahesabiwa kuwa miongoni mwa harakati muhimu sana za Kiislamu nchini Jordan, na chama cha al A'mal al Islami ni tawi la kisiasa la harakati hiyo ya Ikhwanul Muslimin. Chama hiki ndilo kundi kubwa zaidi la upinzani dhidi ya serikali ya Jordan. Chama hicho kilisusia chaguzi za bunge za mwaka 2010 na 2013 kikilalamikia sheria za zamani za uchaguzi zilizobuniwa wakati wa mfumo wa chama kimoja, na kwa madai ya njama ya kufanyika udabanyifu. Wakati huo chama hicho kilitoa wito wa kufanyiwa marekebisho sheria za uchaguzi nchini Jordan. Hata hivyo chama cha al A'mal al Islami kilishiriki uchaguzi wa bunge wa mwaka 2016 na kupata viti 12. 

Sababu ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya Jordan ya kuivunja harakati ya Ikhwanul Muslimin ni ombi la harakati hiyo ya kisiasa dhidi ya Wizara ya Taifa ya Ardhi. Wizara hiyo iliipokonya jumuiya moja iliyoko chini ya harakati hiyo umiliki wa milki na mali zake na kutangaza kuwa, jumuiya hiyo ambayo ilipata kibali cha serikali mwaka 2015, kisheria si sehemu ya Ikhwanul Muslimin. Harakati ya Ikhwanul Muslimin iliamua kuwasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya hatua hiyo ya Wizara ya Taifa ya Ardhi.

Pamoja na hayo Mahakama ya Rufaa ya Jordan imetangaza kuwa sababu ya kuvunjwa kundi la Ikhwanul Muslimin ni kutojulikana hali ya kisheria ya harakati hiyo na kutofungamana kwake na sheria za nchi. Mahakama hiyo imetangaza kuwa, harakati hiyo si kundi halali la kisheria. Maana ya neno "kutojulikana hali ya kisheria ya Ikhwanul Muslimin ya Jordan na kutofungamana na sheria za nchi" ni ishara ya harakati za kundi hilo zinazovuka mpaka na kwenda nje ya Jordan. Tunaweza kusema kuwa, moja kati ya matatizo ya serikali ya Jordan na Ikhwanul Muslimin ni kundi hilo kutofungamana na Katiba ya nchi na taasisi za dola na vilevile fikra na itikadi zake zinazovuka mipaka ya Jordan. Serikli ya Jordan inaamini kuwa, mwenendo huo wa Ikhwanul Muslimin unapingana na maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo.

Nukta nyingine ni kwamba, serikali ya Amman kama zilivyo serikali za Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain inadai kuwa, Ikhwanul Muslimin ina mitazamo na mielekeo ya kigaidi. Kwa msingi huo, japokuwa “kutojulikana hali ya kisheria ya kundi la Ikhwani na kutofungamana na sheria za nchi", kumetajwa na serikali ya Amman kuwa ndiyo sababu ya kuvunjwa kundi hilo lakini inaonekana kuwa serikali ya Jordan imelifungamanisha kundi hilo la lile la Ikhwanul Muslimin la Misri na kulitambua kuwa ni kundi la kigaidi!

Inatupasa kuashiria hapa kwamba, uamuzi huu wa Mahakama ya Rufaa ya Jordan dhidi ya harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo umetolewa sambamba na rai iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Misri kuhusu kiongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo, Muhammad Badie. Mahakama Kuu ya Misri imethibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela aliyopewa kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin pamoja na wenzake watano.

3910857

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha