IQNA

Rais wa Syria: Madola ya Magharibi huwatumia wakimbizi kisiasa

22:58 - November 11, 2020
Habari ID: 3473351
TEHRAN (IQNA) - Rais Bashar al Assad wa Syria amesema Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinawazuia wakimbizi wa Syria wasirudi nchini kwao.

Rais wa Syria ameyasema hayo leo katika mkutano wa kimataifa kuhusu kurejea wakimbizi wa Syria nchini mwao uliofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Damascus. Assad ameeleza kwamba, baadhi ya madola ya Magharibi huwatumia wakimbizi kufikia malengo yao ya kisiasa.

Rais Bashar al Assad amesema, nchi hizo za Magharibi zinatumia mbinu ya kutoa vitisho na kurubuni ili kuwazuia wakimbizi Wasyria wasirudi makwao na akabainisha kuwa, serikali ya Damascus inafanya kila juhudi kwa ajili ya kuwarejesha wakimbizi wote Wasyria nchini humo lakini juhudi hizo zinakabiliwa na vizuizi kadhaa.

Mbali na kueleza kwamba akthari ya Wasyria walioko nje ya nchi wana hamu ya kurejea nchini kwao, Rais wa Syria amezishukuru pia nchi zilizowapokea wakimbizi hao na vilevile misaada iliyotolewa na Iran na Russia kwa ajili ya kupunguza athari za vita na mzingiro iliowekewa Syria, pamoja na jitihada zao za kuwezesha kufanyika mkutano huo wa kimataifa wa Damascus wa wakimbizi Wasyria kurudi nchini kwao.

/3478967

captcha