IQNA

Rais Putin wa Russia atoa wito wa kurejea nyumbani wakimbizi Wasyria

20:16 - November 09, 2020
Habari ID: 3473345
TEHRAN (IQNA) - Mamilioni ya wakimbizi wa Syria ambao walilazimika kutoroka nchi yao kutokana na vita sasa wanapaswa kuwezeshwa kurejea nyumbani kuijenga nchi yao ambayo aghalabu ya maeneo yako sasa yanashuhudia amani.

Akizungumza kwa njia ya video na Rais Bashar al Assad wa Syria Jumatatu, Rais Putin amesema ugaidi wa kimataifa unakaribia kuangamizwa kikamilifu Syria na hivyo Wasyria wanapaswa kuanza maisha yao ya kawaida hatua kwa hatua.

Aidha Putin amesema mapatano ya amani Syria yanapaswa kujumuisha pia kadhia ya kurejea wakimbizi na wale wote waliofurushwa makwao. Ameongeza kuwa mamilioni ya wakimbizi ni watu ambao wako katika umri wa kufanya kazi na kwa msingi huo wanapaswa kurejea na kuanza kujenga upya Syria.

Bado haijabainika iwapo nchi ambazo zina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi Wasyria zitashiriki katika kikao hicho. Tayari Uturuki imeshasema haitashiriki. Syria inaituhumu Uturuki kuwa inawaunga mkono wapinzani wenye silaha ambao wanataka kuiangusha serikali ya Rais Assad. Aidha Uturuki ina askari wake nchini Syria kinyume cha sheria. Lebanon, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, kwa wastani, duniani imesema itatuma ujumbe katika kikao hicho cha Damascus.

Mazungumzo ya Putin na Assad yamefanyika siku mbili kabla ya kongamano la kimataifa la siku mbili ambalo litafanyika katika mji mkuu wa Syria kujadilia kadhia ya wakimbizi. Kongamano hilo linasimamiwa na Russia.

3473071

Kishikizo: Putin syria Assad Wakimbizi
captcha