IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jihadi ya wauguzi katika zama za COVID-19 imewafanya wapendwe zaidi kuliko wakati wowote ule

19:47 - December 20, 2020
Habari ID: 3473475
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemuelezea muuguzi kama malaika wa rehma; na akasema: Katika kipindi cha corona au COVID-19 na katika mazingira magumu mno ya jakamoyo na wasiwasi mkubwa zaidi kuliko ya hali ya kawaida, wauguzi wameweka kumbukumbu ya kazi kubwa na wamejituma na kufanya mambo ambayo kwa kweli ni ya kustaajabisha.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran katika hotuba aliyotoa mubashara kupitia televisheni kwa mnasaba wa maadhimisho ya mazazi ya Bibi Zainab Al Kubra, Salamullahi Alayha na Siku ya Wauguzi.

Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa pongezi kwa wauguzi wote, na mkono wa pole kwa familia azizi ambazo zimeondokewa na wapendwa wao, wauguzi walioaga dunia wakati wakitoa huduma katika kipindi cha janga la corona.

Ameashiria nafasi na mchango wa muuguzi katika kumfanya mgonjwa apate afueni ya kimwili na kiroho na akasema: kwa upande wa nafuu ya kimwili ya mgonjwa, muuguzi ni mshirika na msaidizi wa tabibu na daktari, kwa sababu hata kama daktari atakuwa bingwa na mahiri kiasi gani, lakini kutokuwepo muuguzi kunaweza kutatiza upataji afueni ya kiwiliwili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza pia kwamba, kwa upande wa msaada wa kiroho, tabasamu la muuguzi na au harakati na lugha ya upole na ufariji huwa kwa kweli inamuondolea ghamu na majonzi mgonjwa na kumpa moyo; na hiyo ni moja ya thamani tukufu za Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameeleza jinsi kazi ya wauguzi ilivyo ngumu zaidi na ya wasiwasi mkubwa zaidi katika kipindi cha corona kwa sababu ya uwezekano wa kukumbwa na maradhi na hatari ya maambukizi na akasema: Jihadi iliyofanywa na wauguzi katika wakati huu imewafanya wawe vipenzi zaidi na wenye kuheshimika zaidi mbele ya macho ya watu kuliko wakati wowote ule.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia wajibu na majukumu waliyonayo viongozi wa kuthamini utaabikaji na kujitolea kwa wauguzi na akasisitiza kuwa: kuajiri wauguzi ni mojawapo ya mambo muhimu sana na ya lazima ambalo inapasa lishughulikiwe kwa uzito mkubwa, ili hali ya wauguzi iwe ni ya namna itakayowawezesha kufanya kazi zao kwa usalama; na familia zao pia kutokuwa na wasiwasi wowote juu ya hali zao.

3942124

captcha