IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
8:30 - March 11, 2020
News ID: 3472553
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameafiki pendekezo kuwa, wafanyakazi wa sekta ya afya wanaofariki wakiwa katika mstari wa mbele wa kupambana na ugonjwa wa COVID-19 maarufu kama Corona wahesabiwe kuwa ni mashahidi.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, siku ya Jumanne aliafiki pendekezo la Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki ambaye alipendekeza kuwa 'walinzi wa afya', wakiwemo madaktari, wauguzi, na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya ambao wanapoteza maisha wakiwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya Corona wahesabiwe kuwa ni 'mashahidi katika huduma'.

Wakati huo huo Daktari Namaki amemtumia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kumshukuru kwa kuafiki pendekezo hilo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu laki moja na elfu kumi na tisa wameathiriwa na virusi vya Corona kote duniani na zaidi ya wagonjwa elfu 66 wamepona na kupata shifaa. Zaidi ya 4000 miongoni mwao pia wameaga dunia kutokana na virusi hivyo.

Wizara ya Afya ya Iran imetangaza kuwa hadi kufikia Jumanne watu 2,731 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19, maarufu kama Corona, nchini Iran wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupokea matibabu hospitalini.

Dk Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran akizungumza na waandishi habari Jumanne mjini Tehran amesema hadi sasa watu 8042 wameambukizwa COVID-19 nchini Iran. Aidha amebainisha masikitiko yake kuwa hadi sasa watu 291 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini Iran. 

Hadi hivi sasa virusi hivyo vimeshaenea katika nchi 119 duniani huku idadi ya watu wanaoambukizwa virusi hivyo ndani ya China ikizidi kupungua siku baada ya siku. 

3884377

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: