IQNA

11:28 - March 11, 2021
News ID: 3473725
TEHRAN (IQNA) – Siku kama ya leo miaka 1455 iliyopita, Mtume Mtukufu Muhammad al- Mustafa SAW alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad- Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu yake na Kizazi Chake Kitoharifu- (SAW) alikuwa na umri wa miaka 40.

Tukio hilo adhimu lilijiri  tarehe 27 Rajab Mwaka wa Tembo  wakati Mtume Muhammad SAW alikuwa juu ya kilele cha Mlima Hira, akijishughulisha na ibada ndani ya pango la mlima huo, ambapo ghafla malaika Jibril AS alimteremkia huku akiwa amebeba wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu SW. 

Malaika Jibril alikuwa amebeba ujumbe wa bishara ya Utume kwa Mtume Mtukufu (SAW), ambapo alianza kumsomea aya za mwanzoni za Surat 'Alaq zinazosema: "Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba Mwanadamu katika pande la damu. Soma, na Mola wako ni Mtukufu mno. Ambaye amefunza (kuandika) kwa kalamu. Amemfunza mwanadamu asilolijua." Kwa utaratibu huo, wahyi na Utume, vikawa vimeanza kwa jina la Mwenyezi Mungu na kusoma kwa kalamu, yaani mafundisho yaliyojumuisha tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Maana ya Kubaathiwa

Kubaathiwa kuna maana ya kusimama na kuwa tayari kwa ajili ya kutenda kazi fulani. Na siku ya 'Mab'ath ni siku ambayo, Mtume wa Uislamu Muhammad (SAW), alipewa rasmi Utume. Kutumwa Mtume (SAW) ulikuwa mwanzo wa kumuokoa mwanadamu kutoka katika shirki, kutenda vitendo vilivyo kinyume na uadilifu, ubaguzi, ujinga na ufisadi na kumuongoza kwenye tawhidi, umaanawi, uadilifu na utukufu.

 Aidha kubaathiwa, kuliambatana na kuanza mwamko wa kimaanawi na kuleta mapinduzi katika ulimwengu wa mwanadamu, mapinduzi ambayo athari zake bado zinaendelea kushuhudiwa hadi leo. Mabadiliko haya ya kiroho, yaliwaongoza wanadamu waliokuwa wakiabudu masanamu na kuwaelekeza kwenye chimbuko la maumbile na kuwaonya dhidi ya kufanya matendo machafu, huku na kuwataka wafanye matendo mema.

Siku tukufu zaidi

Siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad (SAW), ulikuwa ni mwanzo wa kumuondoa mwanadamu kutoka katika giza kuelekea kwenye nuru. Ni kwa ajili hiyo ndipo Imam Khomeini MA akaitaja siku hiyo ya kubaathiwa Mtukufu Mtume Muhammad SAW kuwa ni siku tukufu zaidi ulimwenguni. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, siku ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho SAW, hailinganishwi na siku nyingine yoyote ile.

Imam Khomeini amesisitizia suala hilo kwa kusema kuwa, siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad SAW ni siku kubwa ambayo haina mfano wake na wala hapatatokea siku nyingine kama hiyo katika mustakbali. Ni siku ya kubaathiwa Mtume aliyediriki daraja zote za kinafsi na za mbinguni, na akafahamu sheria zote za dhahiri na batini. Kwa ajili hiyo, hakuna haja ya kutumwa ujumbe au Mtume mwingine baada yake.

Kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW, kwa hakika yalikuwa majaaliwa katika historia. Tukio hilo kubwa limebainishwa kwenye aya tukufu aliyoteremshiwa Mtume Mtukufu na kulieleza tukio hilo kuwa ni neema kubwa. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema hivi katika aya ya 164 ya Surat Aal Imraan: 'Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha waumini kwa kuwaletea Mtume miongoni mwao, anayewasomea Aya zake na anayewatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima. Na hakika kabla ya hapo walikuwa katika upotofu wa dhahiri'.

Ukurasa mpya

Kubaathiwa Mtume SAW tunaweza kukutaja kuwa ni kufunguliwa ukurasa mpya katika historia ya mwanadamu, ambapo pia tunaweza kulitaja tukio hilo kuwa ni mapinduzi makubwa yaliyotokea ulimwenguni. Ni vyema kuelewa na kufahamu hali iliyokuwa inatawala katika zama zile za wakati wa kukaribia kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW na adhama ya ujumbe wake huo.

Kabla ya kubaathiwa Mtume SAW ulimwengu uligubikwa na migogoro na mtenguko wa maadili. Ujinga, uporaji, dhuluma na ukandamizaji wa haki za wanyonge na masikini, ufisadi uliochupa mipaka, ubaguzi na vitendo vingine vichafu vilivyokuwa mbali na maadili na ubinadamu, viliigubika jamii ya mwanadamu katika zama hizo.

Katika maeneo yote, eneo la Bara Arabu na hasa katika mji wa Makka kulikuwa na hali mbaya zaidi ya kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi, kijamii na isiyo ya kibinadamu. Heshima ya Waarabu katika zama za ujahiliya huko Makka ilikuwa ni kuyaabudu, kuyataradhia na kuyaomba msaada masanamu yaliyochongwa kwa kutumia miti mikavu, ambapo mtu yeyote mwenye akili, ufahamu na uelewa alishangazwa na kusikitishwa na kitendo hicho.

Zama za Jahiliya (ujinga)

Mwenyezi Mungu SW ameashiria kwenye aya nyingi za Qurani Tukufu baadhi ya mila chafu za kijahiliya na zisizo za kibinadamu na kuwataka watu wajiweke mbali na mila hizo potofu na batili zilizokuwa zimeshika kasi katika zama hizo za ujahiliya.

 Kuna riwaya inayoelezea hali iliyokuwa ikitawala wakati huo huko Saudi Arabia wakati wa kukaribia kubaathiwa Mtume Mtukufu SAW kwa kusema: 'Siku moja Qays bin 'Aswim alikwenda kwa Mtume Mtukufu SAW na kumuambia; Ewe Mtume wa Allah!, Mimi niliwazika wakiwa hai binti zangu wanane wakati wa zama za ujahilia.

 Wakati Qays alipokuwa akimueleza Mtume kisa cha kuwazika binti zake wanane wakiwa hai, Mtume aliathirika mno; kwa kadri kwamba mwili wake ulisisimka na kububujikwa na machozi kutokana na jinsi alivyoathiriwa na kisa hicho na kusema; hiki ni kitendo cha kikatili mno na mtu yeyote katili na asiye na huruma hatopata rehema za Mwenyezi Mungu'.

 

Huenda katika siku hizo hakuna sehemu yoyote ulimwengu iliyokuwa ikiamini hurafa, uchupaji mipaka na ufisadi wa kijamii mithili ya eneo la Hijaaz na Bara Arabu. Waarabu katika zama hizo licha ya kutojua kusoma na kuandika, mitazamo yao pia ilikuwa mbali na mantiki na akili na walikuwa wakifuata na kukumbatia mila, desturi na hurafa zisizo na msingi.

Kuwaongoza watu

 Mtume Mtukufu SAW alitumwa na kupewa ujumbe kwa lengo la kuwaongoza watu waliopotea sio wale tu walioko Bara Arabu, bali kuwaongoza na kuwaokoa watu wote ulimwengu. Ujumbe wa Mtume Mtukufu SAW unaonyesha wazi kwamba ulinganio wake tokea mwanzo ulikuwa umejikita kwenye misingi ya kiakili, kimantiki na dalili. Qurani Tukufu na Mtume Mtukufu SAW wanawataka watu wote kufuata na kukubali kile ambacho kinakubaliana na akili zao.

Miongoni mwa hidaya na zawadi kubwa ya mab'ath na kupewa Utume Bwana Mtume Muhammad SAW ni kupata fursa wanadamu ya kujitakasa, yaani tazkiya. Kwa hakika tazkiya na kujitakasa ndilo lengo kuu la kubaathiwa Mtukufu Mtume (SAW). Neno hilo lina maana ya kuondoka katika kiza cha nafsi na kupambana na matamanio na vishawishi vyote vya ndani kwa ajili ya kuingia katika anga ya usafi wa kimaanawi.

 Chanzo cha tofauti na migogoro yote ambayo inashuhudiwa leo katika jamii ya mwanadamu, kinatokana na ukinzani unaopatikana ndani ya nafsi ya wanadamu. Chanzo cha kuchupa mipaka na kuzuka tofauti kati ya wanadamu, hutokana na nafsi za wanadamu kutotosheka wala kukinai. Kwa hakika suala hilo, linapatikana katika matabaka yote ya watu, wakiwemo wafanyakazi, watu wa vijijini na hata viongozi wenye madaraka ya juu.

Utakaso wa nafsi

Hapana shaka kwamba, kukosekana utakaso wa nafsi kwa viongozi, ni jambo lenye hatari kubwa. Imam Khomeini MA amesema: "Ikiwa watu wa kawaida hawatajitakasa na wakafanya maovu, madhara ya uovu wao huwa na ukomo maalumu. Ikiwa mtu mmoja atafanya uovu sokoni au katika kijiji, inawezekana uovu huo ukawa na athari kwa kiasi fulani tu, lakini ikiwa uovu huo utafanywa na mtu ambaye anakubalika katika jamii ya watu, msomi ambaye watu wamekiri ujuzi wake, viongozi ambao watu wamekubali uongozi wao, watawala ambao watu wamekubali utawala wao, basi wakati huo nchi nzima itaharibika. Hii ni kwa sababu mtu aliyeshika hatamu za uongozi hajatakasika".

Jambo jengine muhimu ambalo ni hidaya na miongoni mwa malengo makuu ya kutumwa Bwana Mtume Muhammad kuwa rehema kwa viumbe wote ni elimu na malezi. Mtume Muhammad SAW alifuatilia na kusisitizia sana suala la kueneza elimu na maarifa sambamba na malezi bora ya kiroho. Qur’ani Tukufu katika aya pili ya Surat Jumu'a inaashiria baadhi ya malengo ya kutumwa Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW kwa kusema: “ Yeye Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, aliyetokana na wao, awasomee Aya Zake, na awatakase, Na awafunze Kitabu na hikima, Japokuwa hapo kabla walikuwa katika upotofu ulio dhahiri.”

 Kwa msingi huo, Mtume Muhammad SAW alikuwa na jukumu la kusoma aya hizo za Mwenyezi Mungu ambazo huinua hadhi ya mwanaadamu ili kutakasa nafsi za watu na kuwaondoa katika dimbwi la upotofu wa shirki na itikadi batili ili waweze kuwa ni wenye akhlaqi au maadili bora. Katika kubainisha lengo hilo Mtume Mtukufu SAW amenukuliwa akisema: “Hakika mimi sikutumwa ila kwa ajili ya kukamilisha maadili mema”

Hivyo kati ya malengo muhimu ya kubaathiwa Mtume wa Mwisho, SAW yametajwa katika Qurani Tukufu kuwa ni pamoja na kutakasa nafsi na kuwalea wanaadamu ili waweze kustawi na kufikia daraja la juu la mwanadamu. Kwa kweli ni chini ya kivuli cha mambo kama hayo ndipo unaporekebishwa na kujengwa uhusiano wa mwanadamu na Muumba wake katika jamii ya Kiislamu.

Ruwaza na kigezo bora

Mtume Muhammad SAW alikuwa ruwaza na kigezo bora zaidi kwa wanaadamu katika upeo wa maadili mema si katika maneno tu, lakini zaidi katika vitendo. Mtukufu huyo aliwaongoza watu na kuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji mafundisho na amali za Kiislamu. Hulka njema na tabia iliyojaa ukarimu ya Mtukufu huyo ni nukta ambazo zilikuwa na mvuto wa kipekee kati ya watu.

 Taathira hii ya kipekee ya akhlaqi bora za Mtume SAW ndiyo nukta ambayo ilipelekkea Waarabu wa zama za ujahiliya au ujinga wajikusanye pembeni mwa mtukufu huyo kwa ajili ya kuchota hazina kubwa ya mafundisho na miongozo mitukufu ya Mwenyezi Mungu kutoka kwa mtukufu huyo.

 Tunamalizia makala hii kwa kukunukulieni tena maneno ya Imam Khomeini, mwanachuoni mkubwa wa zama hizi na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliposema:

 Siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad SAW ni siku kubwa ambayo haina mfano wake na wala hapatatokea siku nyingine kama hiyo katika mustakbali. Ni siku ya kubaathiwa Mtume aliyediriki daraja zote za kinafsi na za mbinguni, na akafahamu sheria zote za dhahiri na batini. Ni kwa ajili hiyo ndio maana hakuna haja ya kutumwa Mtume mwingine yeyote baada yake. 

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: