IQNA

Msafara wa Qur’ani waripoti ukuaji wa asilimia 5 katika shughuli za Arbaeen

15:58 - August 22, 2025
Habari ID: 3481121
IQNA – Waandalizi wa msafara wa Qur’ani kutoka Iran wametangaza ongezeko la asilimia 5 katika shughuli za Qur’ani wakati wa ziyara na matembezi Arbaeen mwaka huu nchini Iraq ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Seyyed Mohammad Moojani, kiongozi wa Kikundi cha Shughuli za Qur’ani cha Kamati ya Utamaduni ya Arbaeen, amesema ongezeko hilo limechangiwa na juhudi za maqari na wahifadhi Qur’ani walioshiriki katika mpango huo.

Akizungumza na IQNA, alieleza kwamba programu hizo ziliandaliwa kwa ushirikiano na Kituo cha Qur’ani cha Astan Quds Razavi katika kipindi cha siku nane nchini Iraq.

“Tuliweza kufanya karibu vikao 1,000 vya Qur’ani, ambavyo vilichangia pakubwa katika kuimarisha safari ya kiroho na ya kidini ya wafanyaziyara wa Arbaeen,” alisema Moojani.

Kwa mujibu wa Moojani, zaidi ya wasomaji 80 wa Qur’ani na vikundi vya Tawasheeh (nyimbo za Kiislamu) walijiunga na msafara wa mwaka huu, wakiwa wanatoka katika mataifa 13 tofauti. Waliendesha shughuli katika njia mbalimbali kuelekea Karbala, zikiwemo Najaf, Diyala, Hilla, Baghdad na Tariq al-Ulama. Shughuli zote zilipangwa mapema na kufanyika kwa ratiba iliyopangwa kwa uratibu maalumu.

Aliongeza kuwa maudhui ya programu yalijikita katika aya za sura za Qur’ani za An-Nasr na Al-Fath, ambazo zilisomwa, kufasiriwa na kushirikishwa kwa mahujaji.

“Kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kiislamu, baadhi ya wahubiri wa Qur’ani wa mpango wa ‘Aya za Kuishi Nazo’ pia walikuwepo Iraq, na waligawa vipeperushi vilivyojumuisha dhana teule za Qur’ani,” alifafanua Moojani.

Jambo la kipekee katika msafara wa mwaka huu, Moojani alisisitiza, lilikuwa ni ushiriki wa kikundi cha wanawake wa Qur’ani kutoka Iran. Kwa muda wa siku sita, walishiriki katika zaidi ya programu 50 za Qur’ani katika vituo vilivyotengwa mahsusi kwa wanawake.

Juhudi zao zilitambuliwa na wasimamizi wa Haram ya Imam Hussein (AS), ambao waliwakaribisha kuendesha kozi za Qur’ani nchini Iraq kwa kipindi chote cha mwaka, alisema.

Ziyara ya Arbaeen, iliyohitimishwa wiki iliyopita, inachukuliwa kuwa miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani. Kila mwaka, mamilioni ya Waislamu wa Kishia kutoka Iraq, Iran na pembe mbalimbali za dunia huenda kwa miguu hadi mjini Karbala kuadhimisha siku ya arobaini tangu kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW).

Zaidi ya watu milioni 21 walihudhuria matembezi ya mwaka huu nchini Iraq.

3494347

Habari zinazohusiana
captcha