Katika taarifa iliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii, kituo hicho chenye makao yake mjini Cairo kimeelezea kitendo hicho kuwa ni cha “uchokozi,” na kikatamka kuwa matukio ya aina hiyo yanapojirudia “huongeza mpasuko ndani ya jamii ya Waingereza.”
Kituo cha AOCE, kilichozinduliwa mwaka 2015 na taasisi ya Al-Azhar ya Misri, huchunguza mienendo ya chuki dhidi ya Uislamu duniani na kufanya kazi ya kuondoa dhana potofu kuhusu dini hiyo.
Tamko hilo limekuja kufuatia tukio lililotokea mapema wiki hii mjini Oxford, ambapo nyama ya nguruwe ilipakwa kwenye vipini vya milango ya msikiti na bendera ya Israeli ikabandikwa katika moja ya milango yake.
Uongozi wa msikiti huo ulithibitisha tukio hilo, ukibainisha kwamba waumini walipatwa na simanzi, lakini bado wamebaki thabiti katika kukuza amani na mshikamano.
Kamishna Mkuu wa Polisi wa Thames Valley, Ben Clark, alilaani kitendo hicho, akikieleza kama “tendo lililokusudiwa kuwadharirisha na kuwavunjia heshima waumini.”
“Hakuna nafasi ya mienendo kama hiyo katika jamii yetu,” alisema, akiahidi kwamba polisi watawafuatilia waliohusika. Doria za ziada zimepelekwa katika eneo hilo ili kuwatia moyo wakazi huku uchunguzi ukiendelea.
Matukio yanayohusisha matumizi ya nyama ya nguruwe yamekuwa sehemu ya mara kwa mara katika uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Uingereza, ikizingatiwa marufuku ya kidini ya Waislamu kula nyama ya nguruwe.
Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakionya kwa muda mrefu juu ya ongezeko la uhasama wa chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza. Taasisi ya ufuatiliaji Tell MAMA UK iliripoti ongezeko kubwa la matukio ya chuki dhidi ya Waislamu katika miaka ya karibuni, ikiwa ni pamoja na ongezeko la asilimia 335 la visa vilivyoripotiwa ndani ya wiki moja baada ya kuzuka kwa vita vya Gaza mwezi Oktoba 2023. Pia wamebainisha vitendo vya mara kwa mara vya unyanyasaji dhidi ya misikiti na taasisi za Kiislamu kote nchini.
Kituo cha Al-Azhar kimekusudia kusisitiza kwamba uhalifu wa chuki wa aina hii hauwaumizi Waislamu pekee, bali pia hutikisa mshikamano wa jamii pana zenye tamaduni na imani mbalimbali.
Mamlaka zimewasihi watu wote wenye taarifa kuhusiana na tukio la Oxford kujitokeza, huku uchunguzi ukiendelea.
3494346