IQNA

12:09 - April 18, 2021
News ID: 3473825
TEHRAN (IQNA)- Washiriki 96 kutoka nchi mbali mbali wanashiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Kusoma Qur’ani (qiraa) ya Televisheni ya Al-Kawthar.

Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha dini na utamaduni katika Televisheni ya Al-Kauthar Sayyid Abbas Razavi, wasomaji Qur’ani wanaoshiriki ni kutoka nchi kama vile Algeria, Morocco, Uturuki, Indonesia, Bahrain, Iran, Iraq, Afghanistan, Ujerumani na Ufaransa.

Amesema takribani wasomaji Qur’ani 250 wamejisajili kushiriki katika mashindano hayo ambapo 96 wameteuliwa kushiriki kwa kuzingatia uwezo wao.

Aidha amesema watu wa kila umri wanaweza kushiriki na hivyo katika mashindano yao mwaka huu kuna mshiriki mwenye umri wa miaka 11 katika Televisheni ya Al-Kauthar inayomilikiwa na Shirika la Utangazaji la Jamhuru ya Kiislamu ya Iran (IRIB)

Razavi amesema Qur’ani Tukufu ni mhimili wa umoja wa Waislamu duniani na hivyo Al-Kauthar TV inatilia maanani sana suala la mashindano ya Qur’ani ambayo ni ishara ya azma ya Iran ya kustawisha na kueneza mafundisho ya Qur’ani.

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ambayo huandaliwa na Televisheni ya Al Kauthar yamepewa aya ya Qur’ani Tukufu isemayo  إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ مَفَازًا , "Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu".  (Qur’ani Tukufu 78:31).

Majaji wa mashindano hayo ni kutoka Iran, Syria, Iraq, Jordan, Misri, Lebanon na Sudan. Majaji hao ni pamoja na Ahmad al Najafi, Rafie al Ameri, Meitham Mumtaz, Natiq Az Zarkani kutoka Iraq, Muutaz Aghai, Mahdi Seif, Sayyid Abbas Anjam, Mohammad Ali Dehdashti na Amir Kismai kutoka Iran. Majaji wengine watakuwa Samii Othmani wa Jordan, Taha Abdul Wahab, Mohammad Kahila na Asfur Mohammad Jabin wa Misri. Aidha wengine watakuwa ni Ridhwan Dariush, Aarif Al Asli na Nurddin Khurshid wa Syria, Adel Khalil na Mustafa Jaafri wa Lebanon na Al Badr Bishara wa Sudan.

Mashindano hayo, ambayo yametajwa kuwa kati ya makubwa zaidi ya aina yake duniani, hufanyika kila mwaka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa njia ya simu au intaneti. Kwa maelezo zaidi kuhusu mashindano hayo, tembelea tovuti ya http://mafaza.alkawthartv.com/

3963993

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: