IQNA

Kongamano la Kimataifa la Quds lafanyika kwa njia ya itaneti

15:34 - May 05, 2021
Habari ID: 3473878
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu limeanza kwa njia ya intaneti ambapo kuna washiriki kutoka nchi mbali mbali.

Kwa mujibu wa taarifa, kongamano hilo ambalo limeanza Jumanne Mei nne linamalizika leo na linahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 30. Miongoni mwa wasomi na wanaharakati wanaozungumza katika kongamano hilo ni kutoka  Iran, Palestina, Malaysia, India, Afghanistan, Pakistan, Ufaransa, Argentina, Iraq, Uturuki, Chile, Imarati, Lebanon, Syria, Uingereza, Canada, na Tunisia.

Kongamano hilo linafanyika kwa njia ya intaneti kutokana na janga la COVID-19.

Waliohutubu katika siku ya kwanza ya kongamano hilo jana ni pamoja na  Ayatollah Alireza Arafi, Mkuu wa Vyuo vya Kiislamu (Hauza) nchini Iran, Sheikh Ahmad Badreddin Hassoun wa Syria, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya Hija Seyyed Abolhassan Navvab, Abdul Hadi Avanj Mohammad wa Malaysia, Katibu wa Kongamano la Intifadha Hossein Amir-Abdullahian wa Iran, Mwakilishi wa Harakati ya Jihad Islamu ya Palestina mjini Tehran, Nasser Abu Sharif  na Soheil Asad wa Argentina.

Kati ya mada kuu ambazo zinajadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na "Palestina na Haki za Binadamu",'Njama za Utawala wa Israel katika kuikalia Quds Tukufu kwa Mabavu', 'Maazimio ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Quds Tukufu' na 'Palestina na Umma wa Kiislamu."

Wakati huo huo, mkuu wa Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu amesema Marekani ilijaribu kusambaratisha kadhia ya ukombozi wa Quds (Jerusalem) kupitia njama mpya katika eneo lakini imefeli kutokana na kuwepo mhimili wa muqawama au mapambano ya Kiislamu.

Katika mahojiano baada ya kuhutubu kwa njia ya video katika kongamano hilo akiwa mjini Qum, Ayatullah Alireza Arafi amesema Wamarekani waliunda kundi la kigaidi la ISIS au Daesh kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu katika eneo. Aidha amesema ule mpango wa kushinikiza nchi za Kiarabu zinazishe uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel zimefanyika kwa lengo hilo hilo hil lakini mipango hiyo haikufanikiwa kutokana na uwepo athirifu wa harakati za mapabano ya Kiislamu.

Ayatullah Arafi aidha amesema kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds katika IRGC, kulifanyika kwa lengo la kusambaratisha mhimili wa muqawama lakini ukweli ni kuwa kuuawa shahidi makamanda wa harakati ya muqawama kumeimarisha zaidi harakati hiyo.

Ikumbukwe kuwa, Imam Khomeini MA Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Waislamu na wapenda haki wamekuwa wakifanya maandamano katika pembe mbalimbali za dunia kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds, na kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi na kikatili zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Quds itakuwa Ijumaa Mei 7.

3474630

Kishikizo: quds kongamano arafi
captcha