IQNA

Kongamano la kimataifa kuwaenzi Waislamu wenye mchango mkubwa, wakiwemo Nasrallah

15:52 - July 27, 2025
Habari ID: 3481007
IQNA – Viongozi wa kidini nchini Iran wametangaza kuanzishwa kwa kongamano la kimataifa litakalowatambua na kuwaheshimu wanazuoni watatu mashuhuri wa Kiislamu ambao urithi wao umeathiri kwa kina fikra za kidini, kitamaduni na kisiasa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu (Hawzah) nchini Iran, alitangaza kuhusu kongamano hilo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Qom mnamo Julai 26.

Kongamano hilo litawakumbuka mashujaa watatu: Shahidi Seyed Hassan Nasrallah, Ayatullah Lotfollah Safi Golpayegani, na Ayatullah Shahrestani.

“Kongamano hili linakusudia kuwatambulisha wanazuoni waliotoa mchango mkubwa katika mandhari ya kijamii, kisiasa na kitamaduni ya eneo letu,” alisema Ayatullah Arafi. Alisisitiza kuwa kongamano hilo litazingatia kwa kina Hawzah za Qom na Najaf, “vituo viwili vya kihistoria vya fikra za Kishia.”

Ayatullah Arafi alieleza kuwa Hawzah hizo mbili zimekuwa na nafasi muhimu katika kuunda mwelekeo wa kisasa wa fikra za Kiislamu. “Watu wakubwa wametoka Qom na Najaf, na athari zao zimefika kila kona ya ulimwengu wa Kiislamu,” aliongeza.

Kongamano hilo litampa heshima maalum Shahidi Seyed Hassan Nasrallah, ambaye alisoma Qom na Najaf na kuathiriwa sana na Ayatullah Mohammad Baqir al-Sadr. Nasrallah anasifiwa kwa upeo wake wa kisiasa na uongozi wake katika harakati za Muqawama. “Uchambuzi wake wa kisiasa ulibadilisha mlingano wa eneo na kumfanya kuwa mtu wa kipekee katika ulimwengu wa Kiislamu,” alisema Arafi.

Nasrallah, kiongozi mashuhuri wa harakati za upinzani za Lebanon, aliuawa katika mashambulizi ya Israel kusini mwa Beirut mnamo Septemba 27, 2024, kufuatia kampeni ya mabomu ya wiki nzima iliyolenga maeneo ya kusini hadi mji mkuu.

Kongamano hilo pia litamtambua Grand Ayatullah Safi Golpayegani, ambaye Arafi alimwelezea kama “nguzo ya elimu ya teolojia, fiqh na itikadi ya Imam Mahdi,” na maandiko yake yanatarajiwa kuchapishwa tena na kutafsiriwa kwa lugha mbalimbali.

Ayatullah Shahrestani, ambaye anajulikana kidogo, atapewa heshima kwa mchango wake wa kihistoria. Kwa mujibu wa katibu wa kongamano hilo, Hujjatul Islam Reza Eskandari, Shahrestani alipambana na ukoloni wa Uingereza karne moja iliyopita akiwa na wanazuoni wa Iraq, akachukua silaha, na baadaye akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu wa Iraq.

“Alianzisha majarida ya Kiislamu, akaunda jumuiya za kielimu Bahrain, India na Yemen, na akaongoza Mahakama Kuu ya Iraq kwa miaka 13,” alisema Eskandari. Licha ya kuwa kipofu kwa miongo mitatu, Shahrestani aliandika vitabu 390, vingi vikiwa bado havijachapishwa, na kuna mpango wa kuvichapisha katika mfululizo wa juzuu 30 zitakazohifadhiwa Kadhimayn.

Eskandari aliongeza kuwa wito wa kuwasilisha makala za kitaaluma umetolewa. Kongamano hilo litakuwa na mikutano ya kisayansi nchini Iran, Iraq na Lebanon, huku taasisi 25 za Kiislamu kutoka nchi hizo tatu zikisaidia mpango huo, na Qom ikiongoza uratibu.

Sherehe za kumbukumbu zimepangwa kwa miaka 2026, 2027, na 2028 kwa ajili ya Nasrallah, Golpayegani, na Shahrestani mtawalia, na tarehe rasmi zitatangazwa hivi karibuni.

3494004

captcha