IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Wananchi watajitokeza kwa wingi kupiga kura iwapo wagombea watawakinaisha

17:04 - May 27, 2021
Habari ID: 3473952
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wananchi wa Iran wapuuze ushawishi wa watu wanaojaribu kuwakatisha tamaa na wanaowaambia hakuna faida kushiriki katika uchaguzi.

Amesema watu hao hawalipendi taifa la Iran. Anayelipenda taifa hawezi kuwazuia wananchi kutumia haki yao ya kuchagua viongozi wao.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo katika mkutano kwa njia ya video kati yake na Spika na Wabunge wa Iran na kusema kuwa, mipango ya wagombea ya kutatua matatizo ya kiuchumi na kimaisha ya wananchi ndiyo sababu kuu itakayowavutia wapiga kura kushiriki kwa wingi katika uchaguzi.

Ameongeza kuwa, bila ya shaka yoyote natija za chaguzi za huko nyuma katika maisha ya watu na ya nchi zitakuwa na athari kubwa kwenye uchaguzi wa mara hii. Amesema: Ni matumaini yetu uchaguzi wa Rais wa tarehe 18 Juni 2021 utalifanya taifa la Iran litoke kifua mbele na utafanyika kwa ufanisi mkubwa tofauti kabisa na wanavyotaka maadui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wabunge waendelee na sifa zao maalumu katika vile kuendeleza harakati ya kimapinduza na ya busara, juhudi zisizosita na utumishi na kushirikishwa kikamilifu wananchi akiongeza kuwa, mabunge yote yanayochaguliwa na wananchi humu nchini lazima yawe ya watu muhimu na wenye ustahiki wa kuwa wabunge wa taifa la Iran kama alivyosisitiza Imam Khomeini, MA.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia baadhi ya wasiwasi uliopo kuhusu uwezekano wa kutojitokeza kwa wingi wananchi katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 18 mwezi ujao wa Juni na kusema, ninavyoamini mimi ni kwamba kiwango cha kujitokeza wananchi katika upigaji kura hakina uhusiano na majina ya wagombea, bali wanachotaka wananchi ni rais anayejua vizuri kuongoza nchi ambaye ataweza kuwatumikia vizuri na kuwatatulia matatizo yao.

3974023

captcha