IQNA

Kiongozi mwandamizi wa Taliban akanusha taarifa kuwa amefariki

23:10 - September 13, 2021
Habari ID: 3474293
TEHRAN (IQNA)- Mwanzilishi mwenza wa kundi Taliban na sasa naibu waziri mkuu wa Afghanistan ametoa taarifa ya sauti Jumatatu akisema alikuwa hai na mzima baada ya habari za kifo chake kuenea kwenye mitandao ya kijamii.

Abdul Ghani Baradar, ambaye wiki iliyopita alitajwa kuwa naibu wa kaimu waziri mkuu Mullah Mohammed Hassan Akhund, alilaumu "propaganda bandia" kwa uvumi wa kifo chake. Ametoa taarifa hiyo kupitia ujumbe wa sauti ambao umesambazwa na utawala wa Taliban.

Mitandao ya kijamii-haswa nchini India, ilikuwa imejaa uvumi kwamba Barada alikuwa amejeruhiwa vibaya katika ufyatulianaji risasi baina ya mirengo hasimu ya Taliban kwenye ikulu ya rais.

"Kulikuwa na habari kwenye vyombo vya habari kuhusu kifo changu," Baradar alisema kwenye ujumbe huo wa sauti.

"Katika usiku wa hivi karibuni nimekuwa nikisafiri. Popote nilipo kwa sasa, sisi sote tuko sawa, ndugu zangu wote na marafiki. Vyombo vya habari kila wakati vinachapisha propaganda bandia. Kwa hivyo, kataa kwa ujasiri uwongo wote huo, na mimi kwa asilimia 100 nakuthibitishia hatuna shida."

Jumapili tarehe 15 mwezi uliopita wa Agosti serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani ilisambaratika na kiongozi huyo kuikimbia nchi baada ya Taliban kuingia Kabul mji mkuu wa Afghanistan. Wachambuzi wa mambo wanasema, hatua ya wanamgambo wa Taliban ya kuudhibiti mji wa Kabul imehitimisha uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa kisingizio cha kuijenga upya Afghanistan.  Aghalabu ya viongozi na wananchi wa Afghanistan wanaamini kuwa, hali ya sasa ya nchi hiyo ni matokeo ya siasa zilizofeli za Marekani nchini humo.

3475703

captcha