IQNA

UNICEF

Mamillioni ya watoto wa Afghanistan hawaendi shule

18:56 - September 19, 2021
Habari ID: 3474314
TEHRAN (IQNA)- Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeripoti kuwa watoto wa Kiafghani zaidi ya milioni nne hawajajiandikisha kuanza shule mwaka huu nchini humo.

Shirika la Unicef limesema kuwa, asilimia 60 ya watoto ambao hawajajiandikisha kuanza shule ni wa jinsia ya kike na kusisitiza kuwa watoto wa Kiafghani hivi sasa wanasumbuliwa na ukosefu wa maji safi, dawa na chakula cha kutosha. Baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kuwaruhusu wanafunzi wa kiume wa shule za sekondari za elimu ya kati na juu pekee kurejea masomoni; Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetaka taasisi za elimu za nchini Afghanistan ziwaruhusu watoto wa kike pia kuhudhuria masomo na kutahadharisha kuwa hatua hiyo itakuwa na taathira mbaya kwa nusu ya jamii ya nchi hiyo. 

Shirika la UNESCO jana liliarifu kuwa, iwapo watoto wa kike wataendelea kuzuiwa  kwenda shule  huko Afghanistan huo utakuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki za msingi za kwenda shule watoto wa kike na wanawake. Shirika la UNESCO limebainisha hayo huku Wizara ya Elimu inayoongozwa na utawala wa kundi la Taliban ikiwa imetoa mwito wa wanafunzi  na walimu wa kiume kudhuhuria mashuleni; huku hatima ya kupata fursa ya kusoma watoto wa kike ikiwa haijulikani. 

Wito wa Taliban

Wakati huo huo, kundi la Taliban nchini Afghanistan limesema kuwa linataka kuwa na uhusiano mzuri na jamii ya kimataifa. Kundi hilo limesema kuwa, manufaa ya Afghanistan ni manufaa ya jamii ya kimataifa na kusisitiza kwamba, lina hamu ya kuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na jamii ya kimataifa.

Matamshi hayo ya Zabihullah Mujahid, msemaji wa kundi la Taliban kuhusu umuhimu wa kuwepo uhusiano mzuri baina ya kundi hilo na jamii ya kimataifa umetolewa katika hali ambayo Taliban wameingia madarakani kwa mtutu wa bunduki na sasa hivi wanataka kuionesha jamii ya kimataifa kwamba kundi hilo limebadilika na kwamba siasa zake sasa si za kutumia mabavu wala mtutu wa bunduki. Katika kipindi cha siku za hivi karibuni, viongozi wa kundi hilo wamekuwa wakitoa misimamo pamoja na kuandika barua mbalimbali kwa sabaha ya kuomba misaada ya kimatiafa ya kifedha na kiuchumi ya kuwawezesha kuendesha serikali.

Kundi la Taliban limeamua kufuata njia ya kidiplomasia katika upeo wa kimataifa kujaribu kuuthibitishia ulimwengu kuwa Taliban wa hivi sasa sio tena wale Taliban wa miaka 20 iliyopita na sasa hivi wana hamu ya kuachana na vita na umwagaji wa damu. Hata hivyo kinachosubiriwa na duru za kimataifa bali hata ndani ya Afghanistan kwenyewe, ni kuona vitendo vya kundi hilo vinabadilika si maneno tu.

Mara baada ya kuiteka Kabul, mji mkuu wa Afghanistan mwezi Agosti,  kundi la Taliban lilitangaza kuwa limekusudia kuunda serikali pana itakayoshirikisha watu wa makundi na matabaka yote ikiwa ni katika juhudi za kuiridhisha jamii ya kimataifa. Lakini si tu halikutekeleza ahadi yake hiyo, bali limeweka pia sheria kali za kukwamisha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kisiasa na kiutamaduni katika jamii ya Afghanistan.

Duru za kimataifa zimekuwa zikisema mara kwa mara kwamba vitendo vya kundi la Taliban ndio msingi wa misimamo ya jamii ya kimataifa na kukubalika kwake kisiasa ndani ya Afghanistan. Iwapo litashindwa kufanya hivyo, kundi hilo litawekewa vikwazo ambavyo vitakwamisha utawala wake. 

3998607/

Kishikizo: taliban ، afghanistan ، watoto
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha