IQNA

Ripoti

Kadhia ya mateka Wapalestina waliotoroka jela ni fedheha kwa Israel

12:44 - September 21, 2021
Habari ID: 3474323
TEHRAN (IQNA0- Mateka 6 wa Kipalestina wametoa pigo kali kwa hadhi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa hatua yao ya kuchimba njia ya chini ya ardhi iliyopewa jina la "Handaki ya Uhuru".

Alfajiri Jumatatu Septemba 6  mateka hao sita walichimba njia ya chini ya ardhi na kufanikiwa kutoroka jela ya Gilboa yenye ulinzi mkali ya utawala haramu wa Israel.

Hata kama wafungwa wote sita waliotoroka wameshakamatwa lakini ujasiri wa kutoroka jela lenye ulinzi mkali ni pigo kubwa kwa usalama wa utawala wa Kizayuni katika pande kadhaa. Kwanza ni kuwa, utawala wa Israel kabla ya tukio hilo ulijaribu pakubwa kuyazuia makundi ya mapambano huko Lebanon na Palestina kuchimba mahandaki na njia za kupitia chini ya ardhi; hata hivyo sasa mateka wa Kipalestina wamefanikiwa kutoka jela ya Israel yenye ullinzi mkali baada ya kuchimba njia ya chini ya ardhi yenye urefu wa makumi ya mita. Kuhusu kutoroka mateka sita wa Kipalestina katika jela ya Gibloa ya utawala wa Kizayuni gazeti la al Quds al Arabi limeripoti kwamba: "Inaonekana kuwa oparesheni hiyo ni kubwa na pana zaidi ya kutoroka mateka hao sita wa Kipalestina; kwa sababu harakati hiyo si pigo kwa walinda jela na uongozi wa jela ya Gilboa peke yao bali ni pigo kwa hadhi na taswira ya serikali mpya ya Naftali Bennet, Waziri Mkuu wa utawala huo; serikali ambayo inakosolewa kwa utendaji dhaifu. 

Mshtuko kwa jeshi la Israel

Pili ni kwamba, kutoroka kwa mateka hao wa Kipalestina katika jela ya Israel kumetokea wakati Wazayuni walipokuwa na wasiwasi wa kutokea machafuko katika eneo la Ukingo wa Magharibi na mipaka ya Ghaza, huku Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizovamiwa na Israel mwaka 1948 wakifanya mikakati ya kuandamana kwa ajili ya kupinga jinai na uhalifu wa Israel. Kutoroka kwa mateka hao wa Palestina katika kipindi ambacho jeshi la Israel lilikuwa limejizatiti kwenye mipaka ya Ghaza na maafisa wa jeshi hilo wakinyimwa haki ya kwenda mapumziko ya "Sherehe ya Mayahudi", kumetambuliwa kuwa ni pigo kubwa lililozusha mshtuko wa aina yake kwa jeshi la Israel. Ukweli ni kwamba, utawala wa Israel haukutarajia kabisa kwamba, unaweza kupata kipigo cha aina hii kutoka kwa mateka wa Kipalestina; na harakati hiyo inaonekana kuwa pigo kubwa la kushtukiza dhidi ya utawala huo. Kwa sababu hiyo vyombo vya habari vimeandika kuwa: "Handaki ya Uhuru imekuwa jinamizi kwa Wazayuni na imeziacha bumbuazi asasi za ujasusi za usalama za Israel."

Uhai mpya kwa harakati za ukombozi wa Palestina

Tatu ni kwamba, Handaki ya Uhuru na kutoroka mateka wa Kipalestina kumetia uhai na msukumo mpya katika mapambano ya kupigania uhuru ya watu wa Palestina. Baada ya tukio hilo, mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Ramon na Negeb walianzisha uasi na kuchoma moto seli kadhaa katika jela hizo. Kwa msingi huo, kutoka huko kumeandaa mazingira ya kujitokeza harakati nyingine kubwa ya mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel. Kwa msingi huo, Israel ambayo ina wasiwasi wa kuibuka machafuko katika jela zake nyingine, imeamua kuwahamishia mamia ya mateka wa Kipalestina katika jela za katikati na kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Tukio la Al Jalbu’a

Israel ina wasiwasi wa kujikariri matukio ya mwaka 1958. Munir Mansour ambaye ni Mkurugenzi wa Jumuiya ya Kuwatetea Mateka wa Kipalestina anasema: Historia ya harakati za mateka wa Kipalesina katika mahabusu za Israel ni ushahidi wa jitihada za muda mrefu za kutoroka jela na mahabusu zenye ulinzi mkali za utawala huo. Miongoni mwa harakati hizo ni ile iliyopewa jina la operesheni ya “Kutoroka Kukubwa” ambayo ilikuwa ya kwanza ya mateka wa Kiarabu na Kipalestina waliotoroka jela ya Shatta karibu na gereza la Al-Jalbu'a hapo mwaka 1958. Wakati huo mateka wa Kiarabu na Kipalestina walipambana na askari magereza wa Israel na kuwapokonya silaha zao kisha wakaua wawili miongoni mwao. Makumi ya mateka wa Kiarabu na Kipalestina walifanikiwa kutoka jela hilo.

Kwa kutilia maanani athari mbaya za operesheni ya Handaki ya Uhuru kwa Israel, inatabiriwa kuwa kuna uwezekano utawala huo ukazidisha ukatili na unyama dhidi ya Wapalestina ili kufidia kipigo hicho dhidi ya vyombo vya usalama vya utawala huo. Kwa sababu hiyo Mustafa al Barghouthi ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Fat’h amesema: Kutokana na kipigo hicho na kufeli kwake baada ya kutoroka mateka sita za Kiplestina, utawala wa Kizayuni yumkini ukamalizia hasira zake kwa mateka wanaoshikiliwa katika jela zake.

Katika upande mwingine hatua ya Israel kuwakamata tena Wapalestina hao mashujaa baada ya kutumia uwezo wa majeshi yake yote na idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani ni jambo lisiloweza kuondoa fedheha na pigo la kiusalama kwa utawala huo bandia.

203084

Kishikizo: palestina ، wafungwa ، ghaza ، israel
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha