IQNA

Jinai za Israel

Wafungwa wa Kipalestina warudi nyumbani, furaha yatanda Ukingo wa Magharibi

22:25 - January 20, 2025
Habari ID: 3480083
IQNA – Jumla ya wanawake na watoto 90 wa Kipalestina waliachiliwa kutoka magereza ya kuogofya ya Israel mapema Jumatatu kama sehemu ya kubadilishana wafungwa iliyohusishwa na makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na utawala haramu wa Israel.

Waliorudi walipokelewa na umati wenye furaha huko Ramallah, ikiwa ni mara ya kwanza kubadilishana tangu makubaliano kuanza kutekelezwa. Kuachiliwa kwa kundi hilo kulifuata kuachiliwa kwa mateka watatu wa Kizayuni huko Gaza saa chache mapema.

Mabasi yanayoendeshwa na Msalaba Mwekundu yalifika Ramallah yakiwa na wanawake 69 na wavulana wa umri wa miaka 12 hadi 21.

Jamaa katika familia, marafiki, na wafuasi walikusanyika kwa maelfu kuwapokea nyumbani licha ya maonyo kutoka kwa mamlaka za Israel dhidi ya sherehe za hadhara.

Miongoni mwa walioachiliwa ni Khalida Jarrar, kiongozi mwandamizi wa Chama cha Ukombozi wa Palestina. Jarrar, mwenye umri wa miaka 62, alikaa miezi sita katika kifungo cha peke yake bila mashtaka rasmi au kesi.

Mwandishi wa habari wa Kipalestina Bushra al-Tawil, aliyekamatwa tangu Machi 2024, pia aliachiliwa.

Akizungumza baada ya kuachiliwa, Tawil alisimulia magumu ya kusubiri uhuru, akisema, “Muda wa kusubiri ulikuwa mgumu sana. Lakini tunamshukuru Mungu, tulikuwa na uhakika kuwa wakati wowote tungeachiliwa.”

Alionyesha matumaini ya kuachiliwa kwa baba yake pia, ambaye anatarajiwa kuachiliwa kama sehemu ya kubadilishana wafungwa inayoendelea.

Miongoni mwa wale waliowapokea wafungwa, Amanda Abu Sharkh kutoka Ramallah alielezea umuhimu wa kihisia wa tukio hilo, akisema, “Wafungwa wote wanaoachiliwa leo wanahisi kama familia kwetu.”

Muhammad, mwenye umri wa miaka 20, ambaye aliachiliwa kutoka kifungo cha Israel, alibainisha furaha yake, huku akieleza kuhusu mateso ya wengi wanaobaki gerezani, wakiwemo wanawake na watoto.

Mabadilishano haya yanawakilisha awamu ya awali ya makubaliano ya kusitisha mapigano, huku mazungumzo zaidi yakitarajiwa.

Hamas imeahidi kuachilia mateka 33 wa Kiyahudi katika wiki zijazo, huku makadirio yakionyesha kuwa hadi Wapalestina 2,000 wanaweza kuachiliwa.

Vita vya mauaji ya kimbari vya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 46,000, na kuwakosesha makazi karibu asilimia 90 ya wakazi wa Gaza.

/3491523

Habari zinazohusiana
captcha