IQNA

Indhari ya Hamas kwa utawala wa Israel kuhusu miamala ya kinyama wanayofanyiwa mateka Wapalestina

21:28 - November 10, 2021
Habari ID: 3474538
TEHRAN (IQNA)- Abdulatif al-Qanua, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu wa Palestina HAMAS ametahadharisha kuwa, hali mbaya ya mazingira yasiyo ya kibinadamu wanayoishi mateka Wapalestina, ambao wanashikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni, yatakuwa cheche itakayowasha moto wa mapigano ya kukabiliana na utawala huo ghasibu.

Kauli hii kwa hakika ni onyo na indhari nyingine kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kwa asasi za kimataifa, ambazo zinapuuza hata haki za kiwango cha chini kabisa za Wapalestina, wakiwemo mateka Wapalestina walioko kwenye jela za utawala wa Kizayuni; kwa sababu katika upeo wa ulimwengu mzima, ni mateka Wapalestina ndio wanaolazimika kutumia kila njia ikiwemo ya kususia kula ili kuweza kuukabili unyama na ukatili unaofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi yao na familia zao.

Onyo jipya la Hamas kwa utawala wa Kizayuni, linafuatia lile la wiki kadhaa nyuma iliyotoa harakati hiyo na ya Jihadul-Islami kwa utawala huo dhalimu kuhusu matokeo hatari utakayokabiliana nayo kutokana na mwenendo wake wa kuendelea kuwatesa na kuwaweka kizuizini Wapalestina kinyume cha sheria. Hamas na Jihadul-Islami zilitoa indhari hiyo na kusisitiza kwamba, kuendelezwa mwenendo huo ni sawa na kukiukwa mstari mwekundu wa harakati hizo za muqawama na zikaeleza bayana kwamba, ikiwa utawala haramu wa Israel utaendelea kufanya hivyo, makundi ya Palestina yatajitoa katika makubaliano yoyote yaliyofikia huko nyuma na utawala huo haramu.

Kuhusu sababu za kushuhudiwa hatua za kihayawani na kiwendawazimu zinazochukuliwa siku hizi na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina ikiwemo kuamiliana kishenzi na mateka Wapalestina, inapasa tuseme kuwa, chanzo cha mienendo hii ya kutapatapa ya Wazayuni ni ushindi mkubwa wa Wapalestina sita, ambao mnamo tarehe 6 Septemba walifanikiwa kutekeleza "operesheni ya njia kwa chini kwa chini" na kutoroka jela ya Gilboa ambayo ni moja ya jela zenye ulinzi mkali zaidi, si katika utawala wa Kizayuni tu, bali hata duniani.

Mafanikio hayo waliyopata mateka hao wa Kipalestina yalitoa pigo kali kwa vyombo vya usalama na intelijensia vya utawala wa Kizayuni na serikali ya waziri mkuu wa utawala huo Naftali Bennett. Kwa muktadha huo tunaweza kusema kwamba, hatua za kinyama zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya mateka Wapalestina ni ulipizaji kisasi kwa Wapalestina sita waliopata ushindi mkubwa ulioudhalilisha utawala ghasibu wa Israel.

4011912

captcha