IQNA

Jihad Islami yalaani safari ya waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel nchini UAE

22:53 - December 13, 2021
Habari ID: 3474670
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Jihad Islami ya kupigania ukombozi wa Palestina imelaani vikali kitendo cha viongozi wa Imarati cha kumpokea nchini humo Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel na kueleza kwamba, hiyo ni khiyana na usaliti kwa taifa la Palestina.

Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ambaye jana usiku aliwasili huko Imarati, leo anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Imarati Mohammed bin Zayed Al-Nahyan na wawili hao kujadilii masuala mbalimbali ukiwemo mkataba wa ushirikiano baina ya pande mbili uliotiwa saini Septemba mwaka jana (2020).

Hii ni safari ya kwanza ya Waziri Mkuu wa Israel kwa mataifa ya Kiarabu yaliyowasaliti Wapalestina na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.

Taarifa ya Jihad Islami ya Palestina imesisitiza kuwa, hatua yoyote ile ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni khiyana na usaliti kwa Palestina.

Itakumbukwa kuwa, Septemba mwaka jana (2020), Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya White House mjini Washington.

Baada ya hapo Sudan na Morocco nazo zikafuata mkumbo huo huo na kutangaza  kuanzisha uhusiano na utawala huo haramu, uamuzi ambao umeendelea kulalamikiwa na kulaaniwa na wapenda haki kote ulimwenguni.

4020481

captcha