IQNA

Mufti wa Quds alaani mbunge wa Marekani aliyetaka Msikiti wa Al Aqsa uvunjwe

18:04 - December 14, 2021
Habari ID: 3474671
TEHRAN (IQNA)- Mufti wa Mji wa Quds (Jerusalem) na Palestina amelaani vikali matamshi ya mbunge mmoja nchini Marekani ambaye ametaka Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds uvunjwe.

Sheikh Muhammad Hussein amelaani matamshi ya kibaguzi ya Paul Gosar, Mjumbe katika Baraza la Wawakilishi la Marekani ambaye ameutaka Umoja wa Mataifa uchukue hatua za kuuvunja Msikiti wa Al Aqsa na kuuhamisha sehemu nyingine.

Matamshi kama hayo yametolewa na kuhani mwenye misimamo ya kufurutu ada Yaakov Hemin. Katika taarifa yake, Sheikh Hussein amesema matamshi hayo ni hatari na ni ya kibaguzi na ni kinyume cha hadhi ya kimataifa ya mji wa Quds na Msikiti wa Al Aqsa.

Amesema  Msikiti wa Al Aqsa,  ni milki ya Waislamu na hakuna anayepaswa kuingilia usimamizi wake na kuongeza kuwa, hujuma yoyote dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ni sawa na kuwatusi Waislamu kote duniani.

Aidha Mufti wa Quds ameitaka jamii ya kimataifa kutekeleza maazimio yote ya Umja wa Mataifa kuhusu Palestina sambamba na kupinga misimamo ya kibaguzi ya utawala ghasibu wa Israell

Msikiti wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu umekuwa ukiandamwa na njama mtawalia za utawala vamizi wa Israel, hatua ambazo zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.

Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kwa kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.

/4020678/

captcha