IQNA

Jua laambatana na Al-Kaaba, likiwapa Waislamu duniani fursa ya kupata mwelekeo Sahihi wa Qibla

19:22 - July 15, 2025
Habari ID: 3480945
IQNA – Jumanne, tarehe 15 Julai 2025, jua limeonekana moja kwa moja juu ya Al-Kaaba huko Makka, hali itakayowawezesha Waislamu kote duniani kuthibitisha mwelekeo wa Qibla kwa usahihi mkubwa.

Saa 6:27 mchana kwa saa za Makka, jua litafika kilele chake moja kwa moja juu ya Kaaba, na kusababisha kutokuwepo kabisa kwa vivuli vya vitu vilivyo wima katika mji huo mtukufu. Tukio hili la nadra la kianga, linalotokea mara mbili kila mwaka, ni fursa ya asili kwa Waislamu wanaotaka kuhakikisha kwa usahihi mwelekeo wa Qibla – yaani mwelekeo wa kuelekea katika Swala.

Mhandisi Majed Abu Zahra, ambaye ni Mkuu wa Jumuiya ya Kianga ya Jeddah, alieleza kuwa tukio hili husababishwa na mwinamo wa mhimili wa Dunia kwa nyuzi 23.5. Jua linapokuwa likirudi kutoka kwenye Tropiki ya Kansa kuelekea ikweta, hupita moja kwa moja katika latitudo ya Makka, ambayo ni nyuzi 21.4 kaskazini.

“Hili hutokea wakati jua linafikia kimo cha nyuzi 89.5,” alisema Abu Zahra, na kuongeza kuwa muda huo hulingana kabisa na adhana ya Swala ya Adhuhuri katika Msikiti Mkuu wa Masjid Al-Haram.

Mara ya mwisho tukio hili lilishuhudiwa tarehe 28 Mei 2025, na halitarudi tena hadi tarehe 16 Julai 2026. Mbali na umuhimu wake wa kidini, tukio hili pia linawapa wanasayansi nafasi ya kuchunguza mienendo ya mwangaza wa jua karibu na kilele (zenith).

Serikali ya Saudi Arabia ilikuwa imepanga kurusha matangazo ya moja kwa moja ya tukio hilo kutoka Msikiti Mkuu wa Makka.

Katika maeneo ya Afrika, Asia, na sehemu za mbali zisizo na teknolojia ya kisasa, waumini wanaweza kutumia nafasi ya jua wakati huo kurekebisha au kuthibitisha mwelekeo wao wa Qibla kwa usahihi wa hali ya juu.

3493849

Kishikizo: makka qibla
captcha