IQNA

Waziri Mkuu wa Pakistan aunga mkono msimamo wa Putin kuhusu Mtume SAW

22:48 - December 26, 2021
Habari ID: 3474726
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ameunga mkono msimamo wa Rais Vladimir Putin wa Russia ambaye amepinga wale wanaomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Imran Khan amesema amekaribisha matamshi ya Rais Putin ambaye amesema kumtusi Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad SAW, si uhuru wa maoni.

Ameongeza kuwa, viongozi wa nchi za Kiislamu wanapaswa kujitahidi kuhakikisha kuwa dunia inafahamu kuwa, kumtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW, si sahihi na kufanya hivyo hakupaswi kutetewa nyuma ya pazia ya ‘uhuru wa maoni’.

Alhamisi  Rais Vladimir Putin wa Russia aliwakosoa vikali wanaomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusema kitendo kama hicho cha kutusi matukufu ya wengine hakiwezi kuhalalishwa kwa kisingizo cha uhuru wa maoni.

Akizungumza na waandishi habari, Putin amesisitiza kuwa kuumiza hisia za waumini kwa jina la uhuru wa sanaa maoni na ni jambo lisiloweza kutetewa hata kidogo.

Katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Magharibi kumeshuhudiwa vitendo vya baadhi ya wasanii hasa wachora vibonzo wakimvunjia heshima Mtume Muhammad SAW kwa kisingizo cha uhuru wa maoni. Vitendo hivyo vimelaaniwa vikali kote duniani na Waislamu pamoja na watetezi wa haki kwa ujumla.

4023461

captcha