IQNA

Idadi ya Misikiti yazidi kuongezeka nchini Russia

19:55 - June 04, 2022
Habari ID: 3475336
TEHRAN (IQNA)- Takriban misikiti 7,500, imefunguliwa katika Shirikisho la Russia au Urusi katika kipindi cha miaka 33 iliyopita.

Hayo ni kwa mujibu wa Mufti Sheikh Talgat Tajuddin, Mkuu wa Kurugenzi Kuu ya Kiroho ya Waislamu wa Russia ambaye ameongeza kuwa katika kipindi hicho pia kumefunguliwa vyuo vikuu saba vya Kiislamu na Akademia ya Kiislamu ya Bulgar.

Ripoti hiyo inaonyesha ongezeko kubwa kutokana na kwamba mwaka 1989, kulikuwa na misikiti 340 tu na vituo viwili vya mafunzo ya Kiislamu katika eneo zima la Shirikisho la Sovieti na karibu nusu misikiti hiyo ilikuwa katika Jamhuri ya Russia. Baada ya kusambaratika Shirikisho la Sovieti na kupanuka zaidi uhuru wa kuabudu, misikiti iliongezeka kwa kasi sana katika Shirikisho la Russia.

Sheikh Tajuddin anasema kuongezeka misikiti na vyuo vya Kiislani ni ushindi sio tu kwa Waislamu bali kwa Russia

Sheikh Tajuddin anaongeza kuhusiana na hilo kwamba rekodi hii ya ujenzi wa misikiti katika Shirikisho la Russia, pamoja na kukua kwa idadi ya makanisa na masinagogi na kutajwa Mwenyezi Mungu Katiba ya Russia ni ishara, ya kuangamia itikadi potovu ya ukanaji Mungu.

Russia ni nchi kubwa zaidi duniani yenye idadi ya watu milioni 146. Uislamu ni dini ya wachache nchini Russia ambapo kuna takriban Waislamu milioni 25. Nchi hiyo ina Waislamu wengi zaidi barani Ulaya. Raia wengi wa Russia ni Wakristo wa dhehebu la Orthodox. Kutokana na idadi kubwa ya Waislamu Russia, nchi hiyo ni mwanachama mwangalizi katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC).

3479166

captcha