IQNA

OIC yataka mazungumzo kutatua mgogoro wa Sudan

17:49 - January 10, 2022
Habari ID: 3474790
TEHRAN (IQNA) – Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetangaza kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada zake za kupatanisha makundi yote ya kisiasa Sudan ili kutatua mgogoro unaoendelea kutokota nchini humo.

OIC imesema kuna haja ya kujumuisha pande zote za Sudan katika mazungumzo ili nchi hiyo ishuhudie amani, demokrasia, usalama na maendeleo.

Katibu Mkuu wa OIC  Hissein Brahim Taha amesema OIC inasimama pamoja na watu wa Sudan ili nchi hiyo iweze kupata uthabiti na umoja.

Kwa mujibu duru za habari, mpango mpya wa Umoja wa Mataifa wa kutatua mgogoro wa Sudan una vipengee vinne ambapo kipengee muhimu zaidi ni kuvunjwa Baraza la Utawala na nafasi yake kuchukuliwa na Baraza la Uongozi litakaloundwa watu watatu wasio wanajeshi.

Mpango huo mpya vile vile umetaka Baraza la Usalama wa Taifa na Ulinzi likabidhiwe kwa wanajeshi lakini baraza hilo liwe chini ya Waziri Mkuu ambaye atakuwa na mamlaka kamili ya uendeshaji kama kuunda serikali huru kikamilifu itakayoshirikisha idadi kubwa ya wanawake.

Kabla ya hapo, Baraza la Utawala la Sudan lilikuwa limepokea vizuri mpango huo wa Umoja wa Mataifa, lakini Chama cha Wafanyakazi ambacho ndicho kilichoko mstari wa bele katika kuhamasisha wananchi kufanya maandamano, kimeupinga.

Mpango huo mpya wa Umoja wa Mataifa umekuja huku wananchi wa Sudan wakiendeleza maandamano yao ya kupinga utawala wa kijeshi na kwa mara nyingine wamewashinikiza wanajeshi warejee makambini na waruhusu raia waendeshe masuala ya kisiasa na kiutawala ya nchi hiyo.

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan ambaye hivi karibuni alitishia kujiuzulu, hatimaye Jumapili alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya waandishi wa habari.

Hii ni katika hali ambayo, katika siku za hivi karibuni, mji mkuu Khartoum na miji mingine ya Sudan imeendelea kushuhudia wimbi kubwa la maandamano ya wananchi ya kulalamikia hali ya kisiasa ya nchi hiyo na kuunga mkono kuweko serikali ya kiraia. Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa tangu jeshi la Sudan litwae madaraka ya nchi Oktoba 25 mwaka jana imepindukia 55.

3477315

Kishikizo: sudan oic
captcha