IQNA

9:45 - February 27, 2022
Habari ID: 3474982
TEHRAN (IQNA)- Babagana Zulum Gavana wa Jimbo la Borno, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria hivi karibuni alionya kuhusu hatari ya kuenea satwa ya kundi la kigaidi la Kiwahhabi la ISIS au Daesh tawi la Afrika Magharibi (ISWAP).

Akizungumza bayana, gavana huyo alisema kundi hilo ambalo limejitenga na kundi jingine la kigaidi la Boko Haram litaibua hatari kubwa ya ugaidi kuliko ile ambayo inashuhudiwa eneo hilo katika kipindi cha miaka 13.  Amesema hali itakuwa mbaya iwapo serikali haitachukua hatua kali dhidi ya kundi la kigaidi la ISWAP ambalo sasa linapanga mikakati mipya ya kutekeleza hujuma.

Gavana Zulum ametoa tahadhari hiyo hiyo hivi karibuni baada ya mkutano wake wa faragha na Rais Muhammadu Buhari mjini Abuja.

Akifafanua kuhusu tishio hilo la ugaidi amesema: "Ongezeko la magaidi wa ISWAP katika baadhi ya maeneo ya jimbo ni la kutia wasiwasi. Hii ni tahadhari ya mapema. Hatupaswi kuruhusu ISWAP kustawi. ISWAP wana uwezo mkubwa, wana kiasi kikubwa cha fedha na pia wana elimu zaidi. Tutafanya kila tuwezalo kuangamiza ISWAP. Kile ambacho Boko Haram wamekuwa wakifanya ni mchezo ukilinganisha na uwezo wa ISWAP."

Kwa miaka 13 sasa, Nigeria imekuwa ikikabiliana na ugaidi wa kundi la Boko Haram hasa katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Taarifa zinasema tokea mwaka 2009 hadi Februari 2022, watu wasiopungua 350,000 wameuawa katika mashambulizi ya Boko Haram huku wengine milioni tatu wakilazimika kuhama makazi yao katika eneo zima la Ziwa Chad. Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto UNICEF linakisia kuwa miongoni mwa waliofariki, laki mbili ni watoto. Aidha uchumi wa eneo hilo umevurugika kabisa kutokana na hujuma za kundi hilo la Boko Haram lenye itikadi za Kiwahhabi. Hivi sasa kumeibuka migawanyiko katika kundi la Boko Haram na kupelekea kujitokeza makundi kinzani ya ISWAP na Ansaru. Makundi hayo ya kigaidi yanashirikiana na maharamia na wahalifu wengine katika kuibua ghasia na kueneza hali ya wahka na woga kote kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Weledi wa mambo wanasema indhari ya Zulum inapaswa kuchukuliwa kwa uzito unaostahiki na serikali ya Rais Buhari ili kukandamiza magaidi hao kabla hawajaimarika.

4037682

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: