IQNA

Rais Ebrahim Raisi

Nchi inahitaji kufuata njia iliyojaa nuru na yenye uwokovu ya Imam Khomeini MA

20:14 - March 10, 2022
Habari ID: 3475029
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hivi sasa, zaidi ya wakati wowote ule, nchi inahitaji kufuata njia iliyojaa nuru na yenye uwokovu ya Imam Khomeini MA.

Rais Raisi ameyasema hayo mapema Alhamisi mjini Tehran wakati wanachama wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomcahgua Kiongozi Muadhamu walipokuwa wamefika katika Haram Takatifu ya Imam Khomeini (MA) kwa lengo la  kujadidisha utiifu wao kwa malengo matakatifu ya mwazilishi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Raisi ameashiria fikra na njia ya hayati Imam na kuongeza kuwa, Iran sasa inahitaji kufuata na kutekeleza kivitendo mafundisho ya hayati Imam ili kwa njia hiyo ustawi wa nchi uweze kudhaminiwa.

Wanachama wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wamelakiwa na Hujjatul Islam wal Muslimin Sayyid Hassan Khomeini walipofika katika Haram Takatifu ya Imam Khomeini MA.

Wakati huo huo Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu lilikamilisha kikao chake cha siku mbili mjini Tehran jana Jumatano kwa kutoa wito wa kumalizika mgogoro wa Russia na Ukraine ambao umekuwa ukiendelea kwa wiki mbili sasa.

Wanachama wa baraza hilo ambalo kwa kawaida hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa wamesisitiza kuwa mgogoro wa Ukraine umetokana na uchochezi wa muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani.  Aidha Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu limekosoa ubaguzi unaoonyeshwa na Umoja wa Mataifa na jamii wa kimataifa kwa ujumla kuhusu vita ambapo kunapigwa kelele kuhusu vita vya Ukraine huku kukiwa na kimya kuhusu jinai zinazotekelezwa dhidi ya watu wa maeneo mengine hasa dhidi ya Wapalestina wanaodhulumiwa. Baraza hilo limesema misimamo kama hiyo inaashiria undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusiana na migogoro ya kibinadamu.

Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran hivi sasa lina wanachama 88 ambao wote ni mafuqaha wa ngazi za juu. Wanachama wa baraza hilo huchaguliwa kwa kupigiwa kura za moja kwa moja za wananchi kwa muhula wa miaka minane.

4041865

captcha