IQNA

Sala ya Ijumaa Tehran

Muelekeo wa kisiasa wa Imam Khomeini (MA) ni kielelezo cha wazi cha falsafa ya siasa katika Uislamu

19:16 - June 03, 2022
Habari ID: 3475329
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo mjini Tehran amesema, muongozo na muelekeo wa kisiasa wa Imam Khomeini -Mwenyezi Mungu Amrehemu- ni kielelezo cha wazi cha falsafa ya siasa katika Uislamu.

Tarehe 14 Khordad 1401 Hijria Shamsia (Juni 4, 2022) ni siku ya Hauli ya Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika hotuba yake ya ibada ya kimaanawi na kisiasa ya Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran, Imamu wa muda wa Sala hiyo Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Mohammad Hassan Abu Turabi Fard ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA) na akaeleza kwamba, Imam Khomeini alifanya jitihada tokea kipindi cha uchipukizi wake kuyafanya maneno ya Imam Ali (AS) kuwa ndio dira ya harakati zake.

Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa Tehran ameashiria maneno ya Imam Khomeini (MA) aliyosema wakati Iran ilipokuwa haijawa na uwezo mkubwa wa kujivunia wa kiulinzi na akasema: Ni kutokana na imani ya yakini aliyokuwa nayo Imam Khomeini ndio maana aliweza kusimama kukabiliana na dunia nzima na akasema, kama nyinyi mtasimama dhidi ya dini yetu, na sisi tutasimama dhidi ya dunia yenu yote.

Halikadhalika, Hujjatul-Islam Abu Turabi Fard amezungumzia uwezo wa kiuhandisi wa Iran na akasema, chini ya mwavuli wa harakati ya kielimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo uwezo wa kiuhandisi nchini, kwa kukiri wananadharia wote duniani, umefikia hatua ya kujivunia, ya kipekee na ya kiwango cha juu.

Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amebainisha kuwa taaluma na elimu ya uhandisi nchini Iran imepiku kasi ya madola yanayotajika, kwa sababu wataalamu na rasilimali watu iliyoandaliwa katika sekta ya uhandisi nchini haina kifani na uwezo wa wataalamu hao umeweza kutumiwa katika nyuga tofauti.

4061788

captcha