IQNA

Iran yawasilisha malalamiko rasmi kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu Sweden

10:34 - April 18, 2022
Habari ID: 3475136
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi mdogo wa Sweden mjini Tehran na kumfahamisha kuhusu malalamiko makali ya Iran kufuatia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kundi moja lenye misimamo mikali nchini Sweden katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mwanadiplomasia huyo wa Sweden aliyeitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumapili amefahamishwa malalamiko makali ya Iran kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden na kundi hilo la misimamo ya kufurutu ada la mrengo wa kulia chini ulinzi wa polisi na kwa kisingizo cha uhuru wa maoni.

Rasmus Paludan, raia wa Denmark ambaye ni kinara wa chama chenye misimamo mikali cha Stram Kurs nchini Sweden alijaribu kuteketeza moto nakala ya Qur'ani Tukufu katika mji wenye Waislamu wengu  siku ya Alhamisi.

Paludan, akiwa ameandamana na maafisa kadhaa wa polisi, alienda katika uwanja uliowazi katika mjiwa Linkoping kusini mwa Sweden ambapo alijaribu kuteketeza moto nakala ya Qur'ani Tukufu. Pludan alikuwa amepanga kuteketeza nakala za Qur'ani katika miji kadhaa ya Sweden wakati wa siku kuu ya pasaka.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetaka Sweden ichukue hatua za haraka na imara kuzuia mipango ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu na kutoa dhamana kuwa vitendo kama hivyo havitakaririwa siku za usoni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekumbusha kuwa, kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu zaidi ya bilioni mbili na kuumiza hisia zao ni utumizi mbaya zaidi wa uhuru wa maoni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imebainisha masikitiko yake kuwa kitendo cha kuivunjia heshima Qur'ani kimefanyika chini ya ulinzi wa polisi ya Sweden na jambo hilo limechafua sura ya Sweden miongoni mwa Waislamu duniani. Kwa upande wake, mwanadiplomasia huyo wa Sweden mjini Tehran amebainisha masikitiko yake kuhusu kintendo hicho na kusema atawajulisha viongozi wa nchi yake kuhusu malalmiko ya Iran.

Jana pia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh alitoa taarifa na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali kitendo cha mbaguzi wa rangi mwenye misimamo ya kufurutu mipaka cha kuchoma moto Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani katika mji wa Linköping nchini Sweden, jambo ambalo limefanyika kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, chini ya mwamvuli na himaya ya polisi wa Sweden."

4050231

captcha