IQNA

Wito wa Hizbullah kuhusu kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, Sweden

17:45 - April 19, 2022
Habari ID: 3475143
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetoa wito kwa Umma mzima wa Kiislamu kuanzisha harakati kubwa zaidi dhidi ya kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani nchini Sweden.

Ni baada ya kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark, Rasmus Paludan, kuchoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu katika mji wa pwani ya Mashariki mwa Sweden wa Linkoping.

Taarifa iliyotolewa na harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani hatua ya watu wenye misimamo mikali nchini Sweden ya kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu, na kulitaja kuwa ni shambulio la wazi dhidi ya imani ya Waislamu, kubeza kwa makusudi dini yao na ni dharau kubwa kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu mambo ambayo hayawezi kuvumiliwa au kufumbiwa macho.

Hizbullah imesisitiza kuwa kitendo hiki kinakariri uovu wa hapo awali na vibonzo vilivyomvunjia heshima Mtume mkubwa zaidi wa Mwenyezi Mungu, Muhammad bin Abdullah (saw).

Katika taarifa yake, Hizbullah imeitaka serikali ya Sweden kuwatia hatiani wahusika wa tukio hilo na kuwachukulia hatua kali zaidi ili kuzuia kukaririwa kwa matukio hayo mabaya.

Hizbullah imeutaka Umma wote wa Kiislamu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na mamlaka za kidini, taasisi za juu za Kiislamu, wanazuoni wa kidini, vyama na makundi ya kisiasa, na jumuiya zote za kimataifa na za kutetea haki za binadamu kuanzisha kampeni pana zaidi ya kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'an Tukufu nchini Sweden.

Awali, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alisema, kukaririwa kwa makusudi kitendo hicho cha dharau katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kumezijeruhi hisia za Waislamu nchini Sweden na kote duniani na kuongeza kuwa: Kitendo hiki cha kuvunjia heshima matukufu ya kidini ni mfano wa wazi wa kueneza chuki na kinapingana na uhuru wa kujieleza. Saeed Khatibzadeh amesisitiza kuwa kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na watu wote wanaoamini fikra ya wanadamu kuishi pamoja kwa amani na mazungumzo baina ya dini mbalimbali.

4050657

captcha