IQNA

Kuvunjiwa heshima Uislamu

Waziri wa zamani Uswidi ataka jinai ya kuteketeza moto Qur'ani Tukufu isitishwe

20:12 - August 19, 2022
Habari ID: 3475647
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Uswidi (Sweden) Jan Eliasson ametoa wito wa kukomesha uchomaji moto wa Qur'ani Tukufu unaofanywa na wafuasi sugu wa siasa kali za mrengo wa kulia, akibainisha kuwa kitendo kama hicho ni sawa na uhalifu chini ya sheria za Uswidi.

"Uchomaji wa Qur'ani unapaswa kuonekana kama uchochezi dhidi ya kundi la watu kulingana na sura ya 16, kipengee 8 cha kanuni za uhalifu," aliandika katika ukurasa wake Twitter siku ya Jumatano.

Maoni hayo yanakuja wakati Rasmus Paludan, kinara wa chama cha mrengo wa kulia cha Denmark Stram Kurs (Msimamo Mkali ) alisema ataendelea kuchoma nakala za Qur'ani Tukufu wakati wa kampeni zake huko Uswidi tena.

Paludan amerudia kitendo hicho cha kuvunjia heshima Uislamu mara kadhaa katika miaka ya nyuma chini ya ulinzi wa polisi wa Uswidi, na kuibua hasira za Waislamu nchini humo na duniani kote. Maandamano kadhaa yamefanyika hadi sasa katika miji tofauti ya Uswidi, na kuwataka viongozi kuacha kuvunjia heshima Uislamu na matukufu yake.

Kulingana na Eliasson, polisi wa nchi hiyo wametumia takriban krona milioni 43 za Uswidi kwa ajili ya kumlinda Paludan na kampeni yake. "Si jambo la busara" kutumia rasilimali kama hizo "kulinda uhalifu ulio wazi," aliongeza.

Pia aliongeza kuwa "chokochoko" hizo zitaondoa heshima ya uhuru wa kujieleza katika nchi hiyo ya Ulaya.

4079137

Kishikizo: sweden ، qurani ، qurani tukufu ، uswidi ، paludan
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha