IQNA

16:01 - May 12, 2022
Habari ID: 3475240
TEHRAN (IQNA)-Mapema jana Jumatano, mwandishi wa habari ya televisheni ya al Jazeera, Shireen Abu Akleh, 51, alipigwa risasi na kuuliwa shahidi kikatili na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati akiwa kwenye kazi yake ya kuripoti uvamizi wa kijeshi wa jeshi la Israel katika kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Jenin.

Jinai hiyo inaendelea kulaaniwa kimataifa huku watetezi wa haki za binadamu wakitaka utawala huo wa Kizayuni wa Israel ufikishwe kizimbani.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali jinai ya utawala haramu wa Israel ya kumuua kwa kupiga risasi Shirin Nasri Abu Aqleh mwandishi habari Mpalestina wa Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar.

Israel ina hofu kuhusu habari za kweli

Saeed Khatibzadeh amesema kuwa, utawala ghasibu wa Israel una hofu na woga wa kutangazwa habari sahihi na za kweli.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia ya shahidi huyo na taifa la Palestina amesema kuwa, hatua hii ya kijinai ya Israel ni ushahidi wa wazi kwamba, utawala huo ghasibu hauheshimu kabisa tasnia ya habari.

Aidha amesema kuwa, kinyume kabisa na madai na propaganda zake, utawala haramu wa israel una woga na wahaka mkubwa wa kutangazwa habar sahihi na ndio maana umefikia hatua ya kumuua kwa kumpiga risasi mwandishi wa habari aliyekuwa katika majukumu yake ya upashaji habari.

Balozi wa Palestina Umoja wa Mataifa amesema, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndio unaohusika na mauaji ya Shahidi Shireen Abu Akleh na akasisitiza kwamba, hawaukubali uchunguzi utakaofanywa na "maafisa wa utawala ghasibu wa Israel" kuhusu mauaji hayo.

Riyadh al-Mansour, balozi wa Palestina Umoja wa Mataifa amewaeleza waandishi wa habari katika makao makuu ya umoja huo mjini New York kwamba, hawakubali uchunguzi wa watu ambao ndio wahalifu waliohusika kumuua shahidi Abu Akleh.

Al-Mansour amesisitiza kuwa, uchunguzi wa Israel hauaminiki na ni wa kubuni na ametaka ufanyike uchunguzi wa taasisi za kimataifa zinazoaminika.

Hamas: Njia ya Abu Akleh iendelezwe

 

Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameulaani vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kumuua shahidi Shireen Abu Akleh mwandishi habari Mpalestina wa Kanali Al Jazeera.

Katika taarifa, Haniya amesema Shireen Abu Akleh alitoa maisha yake muhanga katika njia ya kufichua jinai za kutisha zaidi za Wazayuni katika zama hizi. Ismail Haniya amesema: " Shireen Abu Akleh atakumbukwa miongoni mwa kizazi ambacho kiliendeleza mapambano ya kuwatimua Wazayuni katika ardhi za Palestina." Haniya ameongeza kuwa,  waandishi habari wa Palestina ni walinzi halisi na waendelezaji wa  njia aliyoichukua Shireen Abu Akleh na wengine kabla yake katika vyombo vya habari vya Palestina na hatimaye kuuawa shahidi."

Qatar: Ni ugaidi wa kiserikali

Wakati huo huo Kamati ya Kuunga Mkono Waandishi Habari Wapalestina imetangaza kuwa, lengo la utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuwalenga waandishi habari ni kuzuia kufichuliwa jinai za utawala huo dhidi ya watu madhulumu wa Palestina.

Kwingineko Lolwah Alkhater Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amelaani kitendo cha utawala ghasibu wa Israel kumuua mwandishi huyo wa habari huku akitoa wito wa kuhitimishwa 'ugaidi wa kiserikali wa Israel.

IRIB: Israel haitaki jinai zake ziakisiwe

Wakati huo huo Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) kimelaani vikali jinai ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kumuua shahidi mwandishi habari Mpalestina.

Katika taarifa yake  Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeelezea masikitiko yake sambamba na mshikamano wake na waandishi wa habari huru wa dunia ambao wanatoa taarifa za ukweli na za wazi kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni  na wala hawapuuzi hatua zisizokubalika za utawala huo ghasibu.

Taarifa hiyo imelaani vikali  hatua ya jeshi la Kizayuni ya kuwaua waandishi wa habari ili wasiakisi yale wanayofanyiwa wananchi madhulumu wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hasa  Quds Tukufu (Jerusalem).

Halikadhalika taarifa hiyo imeongeza kuwa, utawala utendao jinai wa Israel si tu kuwa umetanda jinai kama hiyo dhidi ya waandishi habari, bali pia hata madaktari, wauguzi na wengine wengi ambao wamekuwa wakilengwa na vikosi vya utawala wa Kizayuni.

Aidha Kitengo cha Kimataifa cha IRIB kimesema kuuawa Shirin Nasri Abu Aqleh mjini Jenin wakati akitekeleza kazi yake ya upashaji habari, kutabakia hai katika kumbukumbu sawa na walivyobakia hai katika kumbukumbu mashahidi na wahanga wengine wa jinai za utawala wa Kizayui dhidi ya haki za binadamu, ubinadamu na uhuru.

3478864

Kishikizo: Shireen Abu Aqleh ، palestina ، israel ، jinai
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: