IQNA

Idul Ghadir

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu awasamehe wafungwa kwa mnasaba wa Idul Ghadir

11:59 - July 18, 2022
Habari ID: 3475516
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameidhinisha pendekezo la Jaji Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam Hossein Mohseni Ejei la kupunguziwa vifungo au kuachiwa huru wafungwa zaidi ya 2,000 wa Kiirani.

Msamaha huo wa wafungwa 2,272 wa Kiirani waliokuwa wakitumikia vifungo tofauti katika jela za Iran ulitangazwa jana Jumapili na Ofisi ya Ayatullah Ali Khamenei kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Ghadir Khum inayoadhimishwa leo.

Sura ya 110 ya Katiba ya Iran inampa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu haki ya kupunguza au kuwasamehe wafungwa kutokana na pendekezo la Jaji Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran.

Leo Julai 18 inayosadifiana na tarehe 18 Dhul-Hijja mwaka 1443 Hijria ni Sikukuu ya Idd Sayyid Ghadir Khum, moja ya Idd kubwa za Waislamu.

Ghadir Khum ni eneo lililoko baina ya Makka na Madina ambako Mtume Muhammad (S.A.W) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija  kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. 

Siku hiyo Mtume (SAW) alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

IQNA iinatoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu wote duniani kwa kuwadia Sikukuu ya Idd Sayyid Ghadir Khum.

4071545

captcha