IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na Rais wa Uturuki

Shambulio la kijeshi dhidi ya Syria ni hasara ya Uturuki na kwa manufaa ya magaidi

22:30 - July 19, 2022
Habari ID: 3475517
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza ulazima wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kusema: Shambulio lolote la kijeshi katika eneo la kaskazini mwa Syria litazidhuru Uturuki, Syria na eneo zima na Asia Magharibi na kuwanufaisha magaidi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo ​​(Jumanne) katika kikao chake na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na ujumbe aliofuatana nao. Ametilia mkazo umuhimu wa kuongezwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili hususan ushirikiano wa kibiashara na kuutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni miongoni mwa sababu kuu za hitilafu baina ya nchi za Waislamu. Ameongeza kuwa: Marekani na utawala ghasibu wa Israel haziwezi kusimamisha harakati ya kina ya Wapalestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema heshima na utukufu wa Umma wa Kiislamu umo katika kutupilia hitilafu na kuwa macho dhidi ya siasa za mifarakano na akaongeza kuwa: Moja ya sababu za hitilafu na uhasama katika eneo la Magharibi mwa Asia ni utawala ghasibu wa Kizayuni unaoungwa mkono na Marekani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Palestina kuwa ndio kadhia nambari moja ya Ulimwengu wa Kiislamu na akasisitiza kuwa: Licha ya baadhi ya nchi kuukaribisha utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini mataifa ya nchi hizo yanaupinga vikali utawala huo ghasibu.

Huku akisisitiza kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni hazipaswi kutegemewa hata kidogo amesema: Hii leo si utawala wa Kizayuni wala Marekani, wala pande nyingine zinazoweza kusimamisha harakati ya kina ya Wapalestina, na matokeo ya mwisho yatakuwa na manufaa kwa watu wa Palestina.

Akijibu ombi la Rais wa Uturuki la kutaka ushirikiano wa Iran katika kupambana na makundi ya kigaidi, Ayatullah Khamenei amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hakika itashirikiana na Uturuki katika kupambana na ugaidi.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, usalama wa Uturuki na mipaka yake ni usalama wa Iran na kusema: Uturuki inapaswa pia kuutambua usalama wa Syria kuwa ni sawa na usalama wake.

Vilevile ametaja kiwango na ubora wa mabadilishano ya kiuchumi na ushirikiano kati ya Iran na Uturuki kuwa ni mdogo sana ikilinganishwa na uwezo wa pande hizo mbili na kusisitiza kuwa, suala hili linapaswa kutatuliwa katika mazungumzo kati ya marais wa nchi hizo mbili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuongezeka ushirikiano kati ya Iran na Uturuki katika masuala yote ya kieneo ni muhimu na jambo la lazima na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiitetea serikali ya Uturuki katika masuala ya ndani na dhidi ya uingiliaji wa madola ya kigeni.

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki aliwasili Tehran jana usiku akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kwa ajili ya ziara ya siku mbili hapa nchini.

Rais wa Uturuki atashiriki katika Mkutano wa Mchakato wa Amani wa Astana kati ya Marais wa nchi tatu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia na Uturuki. Katika mkutano huo wa pande tatu, marais wa nchi hizo watajadili matukio ya karibuni huko Syria na  mapambano dhidi ya ugaidi. 

4071896

captcha