IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani inapaswa kutimuliwa kutoka eneo la mashariki mwa Furati huko Syria

15:40 - July 20, 2022
Habari ID: 3475519
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jioni ya jana ​​(Jumanne) alifanya mazungmzo na Rais Vladmir Putin wa Russia na ujumbe aliofuatana nao hapa mjini Tehran, ambako amelitaja suala la Syria kuwa muhimu sana na kusema: Suala jingine muhimu katika kadhia ya Syria ni uvamizi wa Wamarekani na kukaliwa kwa mabavu ardhi zenye rutuba na zenye utajiri mkubwa wa mafuta za mashariki mwa Furati (Euphrates), na suala hili linapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa kufukuzwa Wamarekani kwenye eneo hilo.

Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa matukio ya dunia yanadhihirisha haja ya Iran na Russia ya kuzidisha ushirikiana na kuongeza kuwa: Kuna maelewano na mikataba mingi kati ya nchi hizo mbili, ikiwamo katika sekta ya mafuta na gesi, ambayo lazima ifuatiliwe na kutekelezwa hadi mwisho.

Ameutaja ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Russia hasa baada ya vikwazo vya Magharibi kuwa ni muhimu na wenye maslahi kwa nchi zote mbili. Kuhusu matukio ya Ukraine, Ayatullah Khamenei amesema: "Vita ni jambo ngumu na lisilokuwa zuri, na Jamhuri ya Kiislamu haifurahii hata kidogo kwamba watu wa kawaida wanakumbwa na vita, lakini kwa upande wa Ukraine, kama usingechukua hatua, upande wa pili ungesababisha vita."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Wamagharibi wanapinga kikamilifu Russia yenye nguvu na uhuru na ameitaja NATO kuwa ni chombo hatari na kusema: Iwapo njia itakuwa wazi mbele ya NATO, jumuiya hiyo haitambui mipaka, na kama isingezuiwa huko Ukraine, basi hapo baadaye ingeanzisha vita kwa kisingizio cha Cremia. 

Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa: Bila shaka hii leo Marekani na Magharibi ni wadhaifu kuliko hapo awali, na licha ya juhudi na gharama kubwa wanazotumia, mafanikio ya sera zao katika eneo letu yamekuwa finyu sana ikiwemo ni pamoja na huko Syria, Iraq, Lebanon na Palestina.

Amelitaja suala la Syria kuwa ni muhimu sana na kusisitiza msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kupinga mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na ulazima wa kuzuiwa mashambulizi hayo. Amesema: "Suala jingine muhimu katika kadhia ya Syria ni uvamizi wa Marekani na kuyakakalia kwa mabavu maeneo yenye rutuba na utajiri wa mafuta ya mashariki ya Furati (Euphrates); Suala hili linapaswa kutatuliwa kwa kuwafukuza Wamarekani kutoka kwenye eneo hilo."

Ayatullah Ali Khamenei amelaani uingiliaji wa utawala wa Kizayuni katika masuala ya eneo la Magharibi mwa Asia na kupongeza misimamo ya hivi karibuni ya Rais wa Russia dhidi ya Wazayuni. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ushirikiano wa muda mrefu kati ya Iran na Russia kuwa una manufaa makubwa kwa nchi zote mbili na kumwambia Putin kwamba: "Mheshimiwa wewe na Rais wa nchi yetu, wote mna mwelekeo na ufuatiliaji, hivyo ushirikiano kati ya nchi hizi mbili unapaswa kufikia kilele chake katika kipindi hiki."

Ayatullah Khamenei pia amekutaja kuwa macho dhidi ya hadaa ya nchi za Magharibi kuwa ni jambo la lazima na akasema: "Wamarekani ni madhalimu na watu wa hila na hadaa, na moja ya sababu za kuporomoka kwa Umoja wa Kisovieti ni kudanganyika mbele ya sera za Marekani; hata hivyo Russia ya kipindi chako imelinda uhuru na kujitawala kwake."

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran, Rais Vladimir Putin amesema kuhusu matukio ya Ukraine kwamba: "Hakuna mtu anayependelea vita, na kupoteza maisha ya watu wa kawaida ni janga kubwa, lakini tabia ya nchi za Magharibi ilitufanya tusiwe na chaguo ila kuchukua hatua." 

Rais wa Russia ametaja sababu na chanzo cha tofauti kati ya Russia na Ukraine, haswa hatua za kichochezi za nchi za Magharibi na Marekani katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mapinduzi ya Ukraine na sera ya upanuzi ya NATO, licha ya makubaliano ya hapo awali ya kutopanua jumuiya hiyo hadi kwenye mipaka ya Russia na kuongeza kuwa: Baadhi ya nchi za Ulaya zimesema kwamba zilipinga uanachama wa Ukraine katika NATO, na kwamba zilikubali jambo hilo kwa shinikizo la Marekani, na hii inaonesha kwamba nchi hiyo si huru na hazijitawali. 

Rais Vladimir Putin ameyataja mauaji yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni mfano mwingine wa maovu ya Wamarekani. Katika sehemu nyingine ya matamshi yake amezungumzia vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia na kusema: Vikwazo hivi vinazidhuru nchi za Magharibi na matokeo yake ni matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa bei ya mafuta na tatizo la upatikanaji wa chakula.

Putin ameutaja ushirikiano kati ya Rusia na Iran kuwa unaendelea katika sekta na miradi yote na kuongeza kuwa: "Iran na Russia zinapambana na ugaidi kwa pamoja nchini Syria, na katika nyanja ya kijeshi pia tunajaribu kustawisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili na vilevile ushirikiano na mazoezi ya kijeshi pande tatu na China."

4071966

captcha