IQNA

Michezo ya Kiislamu

Michezo ya 5 ya Mshikamano wa Kiislamu inaendelea Konya ya Uturuki

18:55 - August 10, 2022
Habari ID: 3475604
TEHRAN (IQNA) - Mkoa wa Konya wa Uturuki unaandaa toleo la tano la Michezo ya Mshikamano wa Kiislamu, ambayo ilizinduliwa rasmi katika sherehe siku ya Jumanne.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alizindua michezo hiyo baada ya kushiriki katika dhifa ya chakula cha jioni na wawakilishi wa mataifa yaliyoshiriki.

"Ninazindua shughuli za michezo ya Michezo ya 5 ya Mshikamano wa Kiislamu. Nawapongeza wale wote waliochangia kwa niaba yangu na taifa langu. Kila la kheri," Erdogan alisema katika hafla ya ufunguzi.

Zaidi ya wanariadha 4,000 kutoka mataifa 56 wanashiriki mashindano hayo yatakayokamilika Agosti 18. Wanariadha na timu zitachuana katika viwanja 24.

Waziri wa Vijana na Michezo wa Uturuki Mehmet Muharrem Kasapoğlu alisema anaamini kuwa nchi yake ina furaha kuwa mwenyeji wa hafla hiyo, huku akiangazia umuhimu wa michezo.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Hissein Brahim Taha amesema ni muhimu nchi za Kiislamu kuandaa matukio kama hayo ya michezo ambayo yanaimarisha mazungumzo baina ya tamaduni.

Michezo hiyo iliahirishwa kwa mwaka mmoja kutokana na vikwazo vilivyotokana na janga la COVID-19. Mwaka huu, baadhi ya medali 355 zitanyakuliwa kwa wanariadha.

Saudi Arabia iliandaa Michezo ya Mshikamano wa Kiislamu kwa mara ya kwanza mwaka wa 2005. Lengo la michezo hiyo ni kuimarisha ustawi wa wanariadha na kuboresha mshikamano na uhusiano kupitia michezo kati ya nchi za ulimwengu wa Kiislamu. Raia wasio Waislamu wa nchi za Kiislamu pia wanaweza pia kushiriki katika michezo hiyo. Toleo la mwisho la michezo hiyo lilifanyika Baku ya Azabajani mnamo 2017.

Huko Konya, wanariadha watashindana katika michezo kama vile riadha, mpira wa kikapu, soka, mieleka, kunyanyua uzani, mpira wa mikono, judo, karate, kickboxing, tenis, kurusha mishale, taekwondo, voliboli, kuogelea, kurusha mishale ya kitamaduni, n.k

Washiriki watachuana katika michezo hiyo itakayofanyika katika viwanja 12 tofauti kote Konya, vikiwemo viwanja na vituo vya michezo.

3480042

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha