IQNA

Waislamu Uingereza

Msikiti ulioko York nchini Uingereza waalika wasiokuwa Waislamu

18:25 - August 26, 2022
Habari ID: 3475683
TEHRAN (IQNA) – Msikiti mmoja huko York nchini Uingereza unatazamiwa kuandaa siku ya wazi kwa wasiokuwa Waislamu wa eneo hilo kuja kujifunza kuhusu Uislamu na mtindo wake wa Waislamu.

Msikiti na Kituo cha Kiislamu York, huko Bull Lane, Tang Hall, umeandaa siku yake ya kwanza ya wazi kufuatia janga la corona, Jumamosi, Septemba 3, kutoka saa nane hadi  11 mchana.

Siku hiyo ya wazi ni sehemu ya mpango unaofanyika kote  Uingereza wa 'Tembelea Msikiti Wangu', ambao huratibiwa kila  mwaka na Baraza la Waislamu wa Uingereza, ambao utaona zaidi ya misikiti 250 ikifungua milango yake mwishoni mwa juma ili kusaidia kujenga uhusiano mwema na jamii zisizo za Waislamu.

Kura ya maoni ya YouGov iliyofanyika mwaka wa 2018 iligundua kuwa asilimia 70 ya watu Uingereza hawajawahi kutembelea mahali pa ibada isipokuwa kwao wenyewe.

Mohamad Said Douba, katibu wa msikiti, alisema: "Tunataka kukaribisha jumuiya ya ndani ya York, na kuleta kila mtu pamoja ili kujifunza kuhusu maisha ya kila siku ya Muislamu na kuonyesha kile tunachofanya ndani ya msikiti.

"Tunataka kusaidia kukuza maelewano na watu, kujibu maswali ya kawaida na kupambana na kutokuelewana.

"Bila shaka, watu daima wanakaribishwa msikitini siku yoyote wakati wowote."

Wageni watachukuliwa kwenye ziara za kuongozwa kuzunguka msikiti, na wazungumzaji watatoa maelezo yanayofundisha yote kuhusu Uislamu, ikiwa ni pamoja na maonyesho kuhusu Yesu au Nabii Isa katika Uislamu na kipindi cha 'Maswali na Majibu'.

Kutakuwa na vibanda vya utamaduni wa Kiislamu, vikiwamo 'jinsi ya kuvaa hijabu inayovaliwa na wanawake wa Kiislamu, mapambo ya mikono ya hina, viburudisho, shughuli za watoto, na kibanda cha kuwapa wageni fursa ya kuuliza maswali.

Watoto watakuwa wakiigiza, ambayo inasimulia kisa cha mvulana mdogo ambaye anajifunza umuhimu wa kuwa mkweli, akiongozwa na tukio la kihistoria ndani ya Uislamu.

Muumini mmoja katika msikiti huo anayesaidia kuendesha kikundi cha waongofu wanawake alisema: "Nafikiri watu wanatakiwa kuja pamoja, iwe ni watu wa imani tofauti au wasio na imani, hata kama hawapendezwi na Uislamu au dini, kwa sababu watu mara nyingi huwa na imani potofu kuhusu maana ya kuwa Muislamu.

"Nadhani ni muhimu kwetu kutoa nafasi na fursa ya kujaribu kushughulikia hili na kujibu maswali."

Siku hii ya wazi inakuja baada ya ile hafla ya ‘Futari ya Umoja’  ya Msikiti wa York, wakati wa mfungo wao wa  Mwezi wa Ramadhani mwezi Aprili, ambao ulihudhuriwa na zaidi ya watu 400.

Msikiti huomba wageni wavae kwa heshima kama inavyotarajiwa katika sehemu yoyote ya ibada, kama vile nguo zilizolegea, mikono mirefu na suruali ndefu au sketi.

3480222

captcha