IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Waislamu Uingereza wataka waziri mkuu ajaye akabiliane na chuki dhidi ya Uislamu

12:26 - July 16, 2022
Habari ID: 3475509
TEHRAN (IQNA) - Waislamu nchini Uingereza wanataka waziri mkuu ajaye nchini humo akabiliane na chuki ya kimfumo dhidi ya Uislamu katika Chama cha Kihafidhina (Conservative).

Baraza la Waislamu Uingereza (MCB) limesema kuwa waziri mkuu ajaye anahitaji kukabiliana kwa umakini na chuki dhidi ya Uislamu katika "mfumo" wa chama cha Kihafidhina baada ya "kimya cha kutisha " kutoka kwa Waziri Mkuu anayeondoka Boris Johnson.

Zara Mohammed, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu la Uingereza, alisema kwamba Johnson alipaswa kuomba msamaha kwa jamii ya Waislamu katika hotuba yake ya kujiuzulu wiki iliyopita, na kuonya kwamba hakujakuwa na "hatua madhubuti" zilizochukuliwa kukabiliana na chuki ya Uislamu katika chama cha Kihafidhina ambacho pia kinajulikana kama Tory.

Mohammed amesema kwamba MCB imerekodi zaidi ya visa 300 vya chuki dhidi ya Uislamu kwenye chama cha Kihafidhina tangu 2019, na kuongeza kuwa waziri mkuu ajaye "lazima awakilishe kila mtu na haki inatendeka."

Alisema: "Tungependa kuona wagombea hawa wapya wakichukulia suala hili kwa uzito, kwa sababu limekaa sana.

"Tuligundua zaidi ya kesi 300, pamoja na wanachama wakuu wa chama wenyewe wakilalamika juu ya tatizo hili."

Tukio la hivi majuzi katika chama hicho ni pamoja na Mbunge wa Kihafidhina Nusrat Ghani kuripoti kwamba "Uislamu" wake ulikuwa chanzo cha kufutwa kwakekazi kama waziri wa uchukuzi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu la Uingereza aliashiria matamshi machafu ya Johnson alipolinganisha wanawake waliovalia vazi la burqa au niqabu linalotumiwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu kufunika nyusoa na kulifananisha na "masanduku ya barua au vazi la wezi wa benki."

"Bado hatujaona msamaha wowote juu ya hilo," alisema. "Nadhani tamko hilo kwa kweli limewaathiri vibaya wanawake wa Kiislamu.

Amesema baada ya tamko hilo la Johnson, "Tuliona ongezeko la uhalifu wa chuki, hasa dhidi ya wanawake wa Kiislamu ambao walivaa vazi la burqa na mtandio." Aidha amesema matamshi ya Johnson yaliwapa nguvu  wabaguzi wa rangi waliohisi kwamba walikuwa na haki ya kusema mambo kama hayo au kufanya mambo kama hayo dhidi ya Waislamu.

Zara Mohammed, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu la Uingereza amebaini kuwa, “Nadhani wakati umefika tuweze kuona uongozi ambao ni jumuishi, ambao uko tayari kufanya kazi na jumuiya za Kiislamu na jumuiya zote.

"Tunataka kuona hilo hilo katika vyama vyote vya  kisiasa, lakini zaidi katika chama cha Kihafidhina ambacho kinatarajia kuchagua uongozi mpya." Mohammed amemaliza kwa kuhoji, "Je, tunaweza kupata siasa ambayo tunaweza kujivunia, kinyume na uongozi wenye kuleta aibu?"

Msemaji wa serikali ya Uingereza alisema: "Tunachukua mtazamo wa kutovumilia chuki dhidi ya Waislamu kwa namna yoyote ile na tutaendelea kupambana na ubaguzi na kutovumilia."

3479713

captcha