IQNA

Waislamu na Michezo

Wachezaji Waislamu wa Bayern Munich wakataa kupigwa picha wakiwa wameshika Bia.

23:41 - August 31, 2022
Habari ID: 3475713
TEHRAN (IQNA)- Mchezaji wa Morocco Noussair Mazraoui wa Bayern Munich na Msenegali Sadio Mane, ambao ni Waislamu, wamekataa kupiga picha wakiwa wamebeba glasi ya bia katika picha ya kila mwaka ya klabu hiyo ya Bavaria, Ujerumani kutokana na imani yao za kidini.

Kila mwaka, klabu ya Ujerumani hupiga picha ya kitamaduni ya Oktoberfest, kwa ushirikiano na kampuni moja ya kutengeneza bia ya Ujerumani. Oktoberfest ni tamasha la bia la linalofanyika kila mwaka huko Munich.

Klabu hiyo ya Bavaria imetoa picha hizo leo, ikiwa na wachezaji wote wa timu hiyo wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni ya Wajerumani ya Lederhosen.

Wachezaji wote 31, isipokuwa Mazraoui na Mane, kila mmoja alikuwa ameshikilia pombe. Mazraoui alipiga picha huku mikono yake ikiwa nyuma huku fowadi wa Munich Mane akipiga picha huku mikono yake ikiwa chini na huku ikiwa imeshikana pamoja.

Wachezaji hao wawili wa kimataifa wa kandanda ni Waislamu hutekeleza ibada zao hadharani na wametekeleza mafundisho ya Kiislamu ya kutopigia debe pombe.

Mashabiki Waislamu wa kandanda katika mitandao ya kijamii wamepongeza sana hatua ya wawili hao kwa kubaki waaminifu kwa imani yao. "Wameweka dini ya mbele ya wafadhili wowote, tunawapenda na tunawaheshimu zaidi," alisema mtumiaji wa Twitter.

Miaka iliyopita, katika picha sawa na hiyo, Ali Karimi, nyota wa zamani wa Iran wa timu hii ya Munich, pia nayo alikataa kushika bia.

4082270

captcha