IQNA

Njama dhidi ya Iran

Rais Raisi: Adui amefeli katika sera zake za kuidhoofisha Iran

11:20 - November 11, 2022
Habari ID: 3476069
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema njama ya adui ya kuzua ukosefu wa utulivu nchini Iran imefeli sawa na ilivyoshindwa sera ya vikwazo vikali dhidi ya nchi hii.

Raisi aliyasema hayo katika ziara yake katika mji wa Pakdasht, ulioko kusini-mashariki mwa mji mkuu Tehran siku ya Alkhamisi, na kusema kuwa sera ya vikwazo na uvunjifu wa amani ni makosa mawili ambayo adui aliyafanya katika kukabiliana na Wairani, ambayo yote mawili yameshindwa.

Akisisitiza kuwa adui hataki Iran ipate maendeleo na wanasayansi wake wafike katika kilele cha sayansi, Raisi alisema: “Adui anataka matumaini ya watu yageuke kuwa kukata tamaa, adui hataki nchi yetu ipate maendeleo. Sera ya adui ya kuyumbisha nchi ilishindwa kama ilivyoshindwa sera ya vikwazo."

Rais wa Iran aliendelea kusema: "Kwa kusambaratisha vikwazo, tumeuangusha mkakati wa adui."

Akisisitiza kwamba serikali ya Iran imeongeza kiwango cha mauzo ya mafuta ikilinganishwa na wakati kabla ya kuwekewa vikwazo, Raisi alisema, "Walijaribu kuitenga Iran, lakini wao wenyewe wakawa wametengwa. Adui alifikiri kwamba kuwatumikia wananchi kungepunguzwa kwa machafuko na ghasia, lakini ilikuwa ni ndoto tu.”

Aidha amebaini kuwa adui alijaribu kusimamisha maendeleo ya nchi na kuanza kuvuruga usalama, na kuongeza, "Adui anajaribu kutekeleza katika nchi hali ile ile ambayo aliitekeleza katika nchi zingine duniani, lakini hajui kuwa anakariri kosa la kimkakati kwa sababu sera yake ya vikwazo na kuyumbisha nchi imeshindwa tena."

Ghasia zilizuka Iran wiki za hivi karibuni baada ya Bi. Mahsa Amini aliyekuwa umri wa miaka 22 kuanguka katika kituo cha polisi na kufariki akiwa anapata matibabu. Ripoti rasmi ya Idara ya Uchunguzi wa Maiti  ilisema kwamba kifo cha kutatanisha cha Amini kilisababishwa na ugonjwa aliokuwa nao kabla na si kwa kupigwa kichwa au viungo vingine muhimu vya mwili. Baadhi ya wananchi walijitokeza mitaani kulalamikia kifo hicho lakini maandamano hayo yaligeuka na kuwa ghasia zilizochochewa na maadui wa Iran.

Ghasia hizo zilisababisha vifo vya makumi ya watu miongoni mwao wakiemo maafisa wa usalama na watu wasio na hatia. Nchi nyingi za Magharibi zimeonyesha uungaji mkono wao kwa wafanya ghasia katika vitendo ambavyo Tehran inavitaja kuwa vya "kuchochea" ghasia na chuki.

Taarifa ya pamoja ya Wizara ya Intelijensia ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) hivi karibuni imesema mashirika ajinabi ya kijasusi yakiongozwa na Shirika Kuu la Ujasusi la Marekani (CIA) yamekuwa na mchango mkubwa katika kupanga na kuratibu ghasia na fujo zilizoshuhudiwa hapa nchini kwa wiki kadhaa.

4098518

Kishikizo: IRAN ، Ebrahim Raisi ، mahsa amini ، ghasia ، magharibi
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha