IQNA

Fikra za Kiislamu

Bishara njema ya Mwenyezi Mungu kwa wale wanaotoa mali zao katika kutoa sadaka

15:18 - November 13, 2022
Habari ID: 3476079
TEHRAN (IQNA) – Mwenyezi Mungu ameahidi katika Sura Baqarah kuwapa ujira mara mbili wale wanaoshika mikono ya masikini.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, mali ya dunia ni miongoni mwa baraka za Mwenyezi Mungu na kuna maelekezo mengi ya jinsi ya kupata mali na kuitumia.

Kwa mfano, aya ya 31 ya Surah Al-A’raf inasema: “Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu.”

Aya inawausia watu kushika Sala na kutumia baraka za Mwenyezi Mungu huku wakijiepusha na ubadhirifu.

Kwa mujibu wa Tafsir Noor - ufafanuzi wa Kiajemi juu ya Qur'ani Tukufu iliyoandikwa na mwalimu mashuhuri wa Qur'ani Hojat-ol-Islam Mohsen Qara'ati - Quran inaelezea ulimwengu kama mahali pa muda na mtu hapaswi kuiona kama kituo cha kudumu. Wakati huo huo, Qur'an haiwazuii watu kutumia na kufurahia baraka zilizojaaliwa.

Alichoharamisha Mwenyezi Mungu ni kushikamana na dunia na kusahau Akhirah.

Bila shaka, hii haimaanishi kukaa mbali na baraka kutoka kwa Mungu. Aya ya 24 ya Sura At-Tawbah inasema: “Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.”

Aya ina maana kwamba dunia hii ni nzuri maadamu haiwafanyi watu wamsahau Mungu na kuridhika kwake.

Kuna aya zingine zinazoelekeza kwenye njia za kuchangia mali ya mtu kwani kushikamana na mali hii kunaweza kuandaa uwanja wa dhambi.

Aya ya 103 ya Surah At-Tawbah inazungumza na Mtume Muhammad (SAW) akisema: “Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.”

Kwa hiyo, mtu binafsi anayependa mali na akajizuia kutoa Zaka na Khums ataelekea katika kutenda madhambi taratibu.

Wakati huo huo, Quran ina bishara njema kwa wale wakarimu: “Na mfano wa wale wanao toa mali zao kwa kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake mardufu; na hata kama haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.” (Sura Baqarah, aya ya 265)

Kwa mujibu wa aya hiyo, wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu wameahidiwa kuona matokeo ya wema wao huko Akhera. Inabainisha kwamba watu wema wanaosaidia wengine kwa ajili ya Mungu watapata thawabu mbili.

Makala haya yametolewa kutoka katika darsa ya tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya na Hujjatul Islam Muhsim Qara’ati.

captcha