IQNA

Fikra za Kiislamu

Khawf na Raja; Mabawa mawili ya usawa kwa wanadamu

22:57 - November 05, 2022
Habari ID: 3476041
Tehran (IQNA) - Manadamu anahitaji kujua njia ya haki na kuwa na kuwa na mlingano katika chochote anachotaka kufanya. Njia muhimu zaidi ambayo mwanadamu anapaswa kufuata ni ile inayomuelekeza katika wokovu.

Kwenye njia hiyo, kinachosaidia mwanadamu kupata mlingano unaohitajika ni Khawf (hofu) na Raja (tumaini au tarajio) kuhusu Mwenyezi Mungu.

Khawf na Raja ni maneno yaliyo katika Qur’ani na huashiria woga na tumaini wakati huo huo na huunda aina mlingano katika maisha ya mwanadamu. Kwa hivyo mtu anapaswa kuwa na Khawf na Raja kwa wakati mmoja.

Khawf inamaanisha hofu ambayo inatokana na ufahamu. Mtu anajua ni dhambi gani amefanya na anajua kuwa Mwenyezi Mungu ni muadilifu na hutenda haki. Kwa hivyo atakuwa ni mwenye kuhisi aibu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya dhamiri au nafasi yake mwenyewe. Hii ni hali ambayo itaunda aina ya ngao inayomzuia mtu kutenda  dhambi.

Imam Sadiq (SA) alisema: "Muumini daima huwa baina ya hofu mbili. Mojawapo ni hofu ya dhambi zake za zamani, (kwa hivyo) hajui jinsi Mwenyezi Mungu atakavyoamiliana naye. Pili anaogopa hadi mwisho wa maisha yake na hajui dhambi ambazo anaweza kuzifanya ambazo zitasababisha uharibifu wake. Muumini kuwa na hofu katika maisha yake yote, na mambo yake hayaboreki bila woga. "

Raja inamaanisha kuwa na matumaini au matarajio mema. Mtu anajua kuwa iwapo atatubu toba ya hakika baada ya dhambi au makosa aliyotenda basi Mwenyezi Mungu atakubali toba yake. Matumaini haya, pia, yanaunda kizuizi dhidi ya dhambi. Hii ni kwa sababu wakati hana tumaini au tarajio lolote la mustakbali mwema, basi mazuri au mbaya hayana tafauti kwa mtazamo wake na hali hiyo huandaa njia ya kuelekea katika njia ya dhambi zaidi.

Matumaini kuhusu rehema ya Mwenyezi Mungu huweka msingi wa ukuaji na kuelekea ukamilifu kwa sababu mtu anajua kuwa nguvu bora inamuunga mkono.

Khawf na Raja ni mabawa mawili kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu kuelekea ubora na  ukamilifu. Kama vile ndege anapaswa kuwa na mabawa mawili ili apate mlingano sawa na kuweza kuruka, muumini naye anaweza kusonga kwenye njia ya Mwenyezi Mungu ikiwa kuna usawa na mlingano kati ya mabawa mawili ya Khawf na Raja.

Matokeo ya kuwa na Khawf na Raja yanarudi kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu kwa nguzo hizi mbili, hakuna njia nyingine isipokuwa toba, ambayo inabadilisha dhambi kuwa matendo mema.

 “ Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Surah al-Furqan, aya ya 70)

captcha