IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Shahidi ni kielelezo cha "imani ya kweli," "amali njema," na "Jihad katika njia ya Mwenyezi Mungu

16:43 - November 17, 2022
Habari ID: 3476103
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, amesisitiza kuwa, shahidi na kufa shahidi kunaunda jumla ya thamani za kitaifa, kidini, kiutu na kimaadili na kuongeza kuwa: Shahidi ni kielelezo cha "imani ya kweli," "amali njema," na "Jihad katika njia ya Mwenyezi Mungu."

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo katika ujumbe wake kwenye kikao cha watayarishaji wa Kongamano la Mashahidi wa Qum waliokwenda kukutana naye tarehe 30 Oktoba ambao umesomwa leo Alkhamisi kwenye kongamano hilo. Amesisitiza ulazima wa kudumishwa kumbukumbu ya mashahidi na kutangaza ujumbe wao akiutaja mji wa Qum kuwa ni mji wa mapambano. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amezungumzia nafasi na mchango mkubwa wa watu wa Qum katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na katika vita vya kujitetea kutakatifu (vita vya Saddam dhidi ya Iran 1980-1988) na majaribio mtawalia yaliyoikumba nchi hadi hivi sasa, na vilevile umuhimu wa kuonyeshwa sifa bora za mashahidi kupitia lugha ya sanaa na akasema: Kila moja kati ya matukio angavu ya kabla na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ni mithili ya nyota na nukta inayong'aa ya historia; na tukio la (kigaidi) la hivi karibuni huko Shah Cheragh (Shirazi) ni moja ya nyota hizo, ambalo, ingawa limewatia simanzi baadhi ya watu na kuzijaza huzuni na majonzi nyoyo za watu wote, lakini litabakia hai katika historia ya nchi na ni ishara kwamba taifa liko hai na ni chanzo cha fahari.

Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa shahidi na kufa shahidi kunaunda jumla ya thamani za kitaifa, kidini, kiutu na kimaadili na kuongeza kuwa: Shahidi ni kielelezo cha "imani ya kweli," "amali njema," na "Jihad katika njia ya Mwenyezi Mungu", kama ambavyo hii leo, kujitoa mhanga kwa mashahidi, baba na mama zao kumelipa hadhi na utukufu taifa la Iran.

Vilevile amekutaja kuuliwa shahidi kuwa ni dhihirisho la kujitolea mhanga na ushujaa na kuongeza kuwa: Shahidi wa vita vya kujitolea kutakatifu alisabilia maisha yake ili adui muovu na katili asitimize ahadi yake ya kufika Tehran na kulidhalilisha taifa, na shahidi wa usalama anatoa maisha yake kwa ajili ya usalama na faraja ya watu; na kujitolea huku ni kielelezo cha mafundisho yote ya kimaadili yaliyoko ndani ya nafsi ya shahidi na kuuliwa shahidi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuuliwa shahidi kuwa ni kufanya biashara na Mwenyezi Mungu na kudhamini malahi ya kitaifa na kusema: Kuuawa shahidi ni sababu ya mshikamano, na ni kama uzi wa tasbihi unaounganisha pamoja makundi ya makabila na lugha mbalimbali nchini; na katika kila mji kuna majina ya mashahidi mashuhuri ambao waliuawa shahidi kwa lengo moja na katika safu moja na wananchi wenzao kwa ajili ya kuupa izza Uislamu na Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu na kuimarisha Iran. 

4100287

captcha