IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mti imara uliostawi ambao hauwezi kung'olewa

19:38 - October 14, 2022
Habari ID: 3475926
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hautasalimu amri mbele ya madola yenye nguvu na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu hivi sasa imekuwa mti imara uliostawi ambao ni muhali hata kufirikia kwamba unaweza kung'olewa.

Ayatullah Ali Khamenei ambaye alikuwa akihutubia kikao cha maafisa wa viongozi wa nchi na wageni kutoka nchi walioshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu kwa mnasaba sherehe na maadhimisho ya Maulidi na kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) kunakosadifiana na siku ya leo ya tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal na vilevile Imamu Sadiq (as) ameuliza kwamba: "Je, umoja wa Waislamu na kuwa na nafasi ya juu katika ulimwengu wa leo unaobadilika, vinawezekana?", na akasema: Ndiyo, umoja baina ya mataifa ya Kiislamu ni jambo linalowezekana, lakini unahitaji juhudi, bidii na kusimama kidete mbele ya mashinikizo na mashaka."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, katika muktadha huo, matumaini makubwa zaidi yako kwa vinara wa ulimwengu wa Kiislamu na vijana walioelimika na mchango wao katika kuongoza fikra za Umma. Ameongeza kuwa: Mfano wa uwezekano wa kuathiri ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo mche huo mdogo ulisimama imara dhidi ya madola mawili makubwa ya wakati huo chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini (ra) na kwamba mche huo sasa umegeuka na kuwa mti mkubwa ambao ni kosa hata kwa mtu kudhani kwamba anaweza kuung'oa.

Ayatullah Khamenei amesema: "Sisi tumesimama imara na kusonga mbele; hata hivyo  kusimama kidete, kama ilivyo kazi nyingine yoyote, kuna mashaka yake, lakini pia wale wanaosalimu amri wanakumbana na mashaka, na tofauti iliyopo ni kwamba kusimama kidete kunamfikisha mtu kwenye maendeleo, na kusalimu amri kunamrudisha nyuma."

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja suala la baadhi ya nchi za Waislamu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni miongoni mwa usaliti mkubwa zaidi na kusema: Huenda baadhi wakasema kuwa kupatikana umoja katika hali ya sasa hakuwezekani kutokana na kuwepo baadhi ya viongozi katika nchi za Kiislamu, lakini wasomi, maulamaa na wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu wanaweza kuyafanya mazingira ya sasa kuwa tofauti na matakwa ya adui, na wakati huo itakuwa rahisi kujenga umoja baina ya mataifa ya Waislamu.

Ayatullah Ali Khamenei ameeleza masikitiko yake kutokana na jinai zinazofanywa na kundi la Daesh huko Iraq, Syria na hasa mauaji ya wanafunzi nchini Afghanistan na kuongeza kuwa: Kuna watu wenye misimamo mikali katika pande zote mbili za Shia na Suni ambao hawana uhusiano wowote na Ushia wala Usuni, na misimamo hiyo mikali haipaswi kutengeneza mazingira ya kushutumu misingi ya madhehebu tofauti; hivyo kuna udharura wa kupambana vikali na wale wanaochochea hisia za upande mwingine kwa kutumia kisingizio cha kutetea madhehebu nyingine.

Amesema kuongezeka matatizo, mashinikizo na mauaji huko Palestina na sehemu nyinginezo za Ulimwengu wa Kiislamu ni matokeo ya "mgawanyiko wa Umma wa Kiislamu". Ameashiria mambo mengi yanayowakutanisha pamoja Waislamu na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya kila iwezalo kwa ajili ya kutimiza kivitendo umoja wa Kiislamu na mfano wa wazi wa jambo hilo ni uungaji mkono na misaada yake ya pande zote kwa ndugu zetu wa Kisuni huko Palestina, na msaada huu utaendelea kwa nguuvu zote."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kambi ya mapambano na muqawama iliyoibuka katika Ulimwengu wa Kiislamu inaungwa mkono na Jamhuri ya Kiislamu na kueleza kuwa: Tuna imani kwa rehma na msaada wa Mwenyezi Mungu na tuna matumaini ya kutimizwa kivitendo lengo kubwa la kuwepo umoja wa Kiislamu.

4091739

captcha